WAZAZI WAASWA KUTOA  MAFUNZO YA DINI KWA WATOTO

Na waandishi wetu Musoma.
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuwa mfano kwa kuwahamasisha watoto kusali kwenye familia, jumuiya, kanisani pamoja na kuonesha matendo ya huruma katika kuwajenga kiimani na upendo ili kukabiliana na magumu yanayotoka katika familia. 
Wito huo umetolewa na Paroko wa parokia ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu Jimbo Katoliki Musoma padri Benedict Luzangi katika Misa ya sikukuu ya familia Takatifu ya Yesu, Maria na Joseph ambayo imeambatana na utoaji wa sakramenti ya ubatizo kwa watoto 28. 
Padri Luzangi amesema kuwa familia ni kitovu cha maisha ya fadhila ambayo huleta umoja, upendo, uwajibikaji, imani na malezi bora ya kiimani.
Hata hivyo padri Luzangi amekemea tabia ya baadhi ya wazazi wasioona uchungu wa familia za watu wengine hasa wanapokuwa na shida pia wasiotunza na kuwajali wazee kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kupungukiwa na imani kama mkristo  na kwamba mali  na utajiri bila furaha ni sawa na bure. 
Kwa upande wao wazazi na walezi wa watoto hao kwa nyakati tofauti wameahidi kuwalea watoto katika misingi bora ya kidini na kuwaandalia maisha bora ya kiroho na kimwili yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, paroko msaidizi wa parokia ya Mugango, Padri Cleophas Sabure amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto kulingana na maisha yao pasipo kutamani vitu wasivyokuwa na uwezo navyo kwa kuwa jamii na Kanisa wanategemeana katika masuala mbalimbali ya kiimani, kiuchumi na kimaendeleo na kuwakumbusha kujitathimini ili kuona walichokifanya katika mwaka 2017.
Wakati huo huo, jumla ya ndoa 14 zimefungwa katika maadhimisho ya sikukuu ya familia Takatifu katika Parokia ya Kiabakari jimboni Musoma. 
Maadhimisho hayo  ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila na paroko wa parokia ya Kiabakari padri  Wojciech Adam na kuhudhuriwa na waamini zaidi ya 600 katika Kanisa hilo la Huruma ya Mungu Kiabakari.
Askofu Msonganzila amewaasa wanandao hao kuiga familia Takatifu ya Yosefu, Maria na mtoto Yesu kwa kuishi katika nguzo tatu ambazo ni ndoa, kufanya kazi kwa pamoja kama ilivyokuwa kwa mtoto Yesu na wazazi wake na  kuishi katika sala na kuwafundisha watoto wao sala na kuwa na moyo wa shukrani katika maisha yao.
Amesema sala ni kiungo kishikamanishi katika familia na hatimaye hujenga familia iliyo bora na ya kumpendeza Mungu, hivyo familia ijikite zaidi katika kusali hasa kuwapeleka watoto wao kanisani na kula nao pamoja na siyo kuwaacha wakishinda katika mitandao ya kijamii ambayo itawapoteza kimaadili. 

Amewausia wanandoa hao kuwa na upendo wa kweli katika ndoa hasa kuvumilia, kunyenyekea, kushirikiana na kusameheana pindi wanapokosana au kukwaruzana na palipo na shida wasisite kutafuta ushauri.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU