Askofu Msonganzila akemea ukatili kwa watoto

Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amekemea ukatili unaoendelea kwa watoto katika jamii akisema kuwa ni unyama kwa watoto ambao hawawezi kujitetea.
Askofu Msonganzila ameyasema hayo hivi karibu katika Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka 2017 salama na kuvuka mwaka mpya salama,  iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Maria Mtakatifu Mama wa Mungu.
Amesema kuwa, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili kwa watoto wadogo ambavyo vinahusishwa na  chuki na hasira ambavyo vyote ni  kinyume na mapenzi ya Mungu  na uumbaji.  
“Matendo ya kikatili kwa watoto yanazidi kuongezeka kwa kasi, tunamtesa mtoto kwa kumchoma moto kwa kupoteza shilingi 100 au kwa kulamba sukari.
Nani asiyefahamu maumivu ya moto? Ni mateso makali sana. Mtoto wa miaka miwili ama mitatu unamchoma kwa nini usimuonye kwa kumkemea au kumpa adhabu inayoendana na umri wake?
Wakristo wenzangu watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, wadogo hawa hawana pa kukimbilia,” amesema.
 Amesema hakubali wala hatambui kauli inayosema ‘Watoto wa mitaani’ kwani hakuna mtoto wa mitaani, wanaokuwepo mtaani wamekimbia mateso nyumbani.
“Naombeni sana kila mmoja atumie siku hii kuomba toba, kujitakasa na kama mtu amethubutu kushiriki kutoa mimba hata awe mume naombeni sana mtubu dhambi ili kuanza mwaka kwa amani na utulivu “alisema Askofu Msonganzila.
Aliwaomba waamini wa Jimbo hilo kuhakikisha wanapunguza mizigo mingi ya hasira ambayo ndio inayosababisha matendo ya kinyama  yakiwemo mauaji yasiyo na hatia, ukatili kwa watoto wadogo na wanawake pamoja na ugomvi ndani ya jumuiya na familia zao. 
“Ugomvi, chuki na na hasira ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani, ndugu zangu tusikubali kubeba kilo 100 za hasira maana ukiwa na hasira na usijue kuizuia hasira yako unaweza kusababisha mambo mabaya yasiyompendeza Mungu.
Tujitahidi mwaka huu uwe mwaka wa baraka na mafanikio kwa kila mmoja wetu, kwa kuanza kuweka mipango mizuri ndani ya familia zetu na kukemea vitendo vya ukatili katika jamii yetu,” amesema Askofu  Msonganzila.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU