Msalaba wa Jubilei Bagamoyo ni shule ya matumaini
MSALABA wa Jubilei
ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara unaozungushwa kwenye parokia tatu za
Bagamoyo ni shule ya matumaini. Mwaka 2017 Askofu Telesphor Mkude Askofu wa
Jimbo Katoliki la Morogoro alizindua Msalaba wa Jubilei ambao ulitakiwa
kutembezwa katika parokia zote za Bagamoyo: Parokia ya Epifania, Parokia ya
Moyo Safi wa Bikira Maria na Parokia ya Kristo Mfalme.
Bado msalaba
unatembezwa katika parokia hizi. Msalaba huu utukumbushe siku ya Ijumaa Kuu
Yesu Kristo alipokufa msalabani na kuzikwa baadaye alifufuka. Ukweli huu
unatupa matumaini: hakuna Jumapili ya Pasaka bila Ijumaa Kuu, hakuna taji la
utukufu bila taji la miiba, baada ya dhiki faraja.
Padre Raniero
Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya kipapa alisema siku ya Ijumaa Kuu tarehe 14
Aprili 2017 kuwa, “Msalaba ni tumaini la pekee duniani”. Msalaba wa Kristo ni
ujumbe wa Mungu wa “I love You.” “Mungu alituthibitishia upendo wake
msalabani wakati Kristo aliponing’inia na kuvuja damu na kufa, ni Mungu alikuwa
anaiambia dunia, ‘Nakupenda,” alisema mchungaji Billy Graham. Ukweli huu
unatupa matumaini.
Yesu akiwa msalabani aliambiwa maneno
saba. Neno la tatu kwa Yesu msalabani lilitoka kwa mwizi ambaye katika mapokeo
ya Kanisa Katoliki anaitwa Dismas au Demacus. Huyu alikuwa upande wa kulia wa
Yesu. Neno lake lilikuwa ni sala. Aliomba mara moja maishani akapata. Alitafuta
mara moja maishani akapata. Alibisha hodi mara moja maishani mlango
ukafunguliwa. Lakini tukumbuke bahati ya mwenzako isikulaze mlango wazi.
Dismasi alisema:
“Unikumbuke Bwana katika ufalme wako.” Sala ya unikumbuke mimi, ni sala ya
imani. Sala ya unikumbuke mimi, ni sala ya matumaini. Sala hiyo inafunua imani
katika Kristo kama mfalme wa kweli. Yesu kweli anaweza kuokoa, hata kama
hajiokoi mwenyewe – wala mhalifu kutoka msalabani.
Maneno ya mwizi
Dismasi msalabani yalikuwa neno la imani, matumaini na upendo. Juu ya hili Baba
wa Kanisa Gregori alikuwa na haya ya kusema: “Fadhila tatu ambazo mitume
walizungumzia mwizi akiwa amejaa neema alizipokea na kuzitunza pale msalabani.
Mfano alikuwa na imani kwa Mungu atatawala ambaye alimuona kufani kama yeye.
Alikuwa na matumaini yeye ambaye aliomba kuingizwa katika ufalme Wake. Alitunza
fadhila ya ukarimu kwa ari katika kifo chake, alimkosoa ndugu yake na mwenzi
mwenzi ambaye alikuwa kufani kwa kosa kama lake.”
Mwizi Dismasi
alitumia vizuri talanta zake pale msalabani. Alitumia talanta ya mdomo. Mikono
na miguu vilikuwa vimefungwa. Mwili wake ulikuwa umefungiwa msalabani. Ulimi
wake ulikuwa uko huru. Aliutumia kusali. Aliutumia kumwonya mwizi mwenzake na
kumshauri. Alitumia ulimi wake kutubu. Moyo wa mwizi ulikuwa
hukufungwa. Mwizi alitumia moyo kuamini matendo ya haki. Huu ni mtazamo wa Baba
wa Kanisa Mtakatifu Gregori.
Alikuwa na haya ya
kusema: “Msalabani misumari ilifunga mikono yake na miguu yake hakuna sehemu
ambayo ilibaki huru bila kuteswa isipokuwa moyo na ulimi wake. Kwa mwanga wa
Mungu, mwizi alimtolea chochote kilichokuwa huru, kama ilivyoandikwa, kwa moyo
ili aamini matendo ya haki, kwa mdomo ili atubu kwa ajili ya wokovu.”
Padri Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa
nyumba ya kipapa alisema haya juu ya mwizi mwema, “hakuna sababu msingi ya
kumkatia Mungu matumaini kama ilivyokuwa kwa Kaini na badala yake, watu wawe na
matumaini thabiti kama ilivyojionesha kwa yule Mwizi mwema, aliyetambua dhambi
zake na kuomba msamaha, lakini Kaini aliona ukubwa wa dhambi akashindwa kuomba
toba na msamaha.
Msalaba duniani ni
kielelezo cha mateso na mahangaiko yote ya binadamu na daima utaendelea kuwa ni
sehemu ya historia ya maisha ya binadamu, kwani Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanaye
wa pekee ulimwengu si kwa ajili ya kuhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe
katika yeye.”
Mmoja wa wale
wahalifu waliotundikwa alimtukana akisema, “Je, wewe si Kristo? Basi, jiokoe
mwenyewe na sisi pia” (Luka 23: 39). Mateso ni mtazamo. Mateso msalabani
yalimfanya mwizi mkono wa kushoto avunjike moyo, lakini yalimfanya mwizi mkono
wa kulia avunje rekodi-mwizi aliyeiba mbingu.
Watu wanaweza kuwa na
mateso yaleyale, tofauti ni mtazamo walio nao juu ya mateso hayo. Askofu Fulton
Sheen alikuwa na haya ya kusema: “Watu wanaweza kuwa katika mazingira
yanayofanana na kutenda namna tofauti kabisa. Wezi wote walifanana katika
walichokikosa moyoni na bado walimtendea tofauti mtu aliyekuwa katikati yao.
Njia za nje, mfano mzuri kwa vyenyewe havitoshi kumbadilisha mtu, moyo
usipobadilika.”
Ni moyo unaompeleka
mtu mbinguni. Ni moyo unaompeleka mtu motoni. Mwizi upande wa kushoto alikuwa
na mtazamo hasi. Mwizi upande wa kulia alikuwa na mtazamo chanya. Mwizi upande
wa kushoto alimuona Yesu mfanya mazingaombwe ambaye angempa ukombozi wa
kimwili. “Wokovu tu ambao mwizi upande wa kushoto angeelewa haukuwa wa kiroho
au kimaadili, bali kimwili: ‘Jiokoe na utuokoe sisi!’
Okoa nini? Roho zetu?
Hapana! Mtu hana roho! Okoa miili yetu! Dini ina faida gani kama haiwezi
kuondoa maumivu?” alisema Askofu Fulton Sheen. Kuna ambao wanaona dini kama
Hospitali ya Rufaa. Isipotibu na kuponya magonjwa ya kimwili wanaiacha na
kutafuta dini nyingine. Huu ni mtazamo. Binadamu ana roho na mwili. Dini ni Hospitali ya wadhambi.
Comments
Post a Comment