Bweni lateketea, Biblia na Rozari pekee vyasalia

Mwanafunzi wa Seminari ndogo ya St. Mary Mbeya akionyesha Biblia Takatifu iliyosalimika mara baada ya moto kuteketeza vifaa vilivyokuwa katika moja ya mabweni seminarini hapo hivi karibuni (Picha zote na Thompson Mpanji)


Baadhi ya vifaa vilivyoteketea kwa moto lakini Biblia na Rozali zilikutwa salama


Hata baada ya moto kuteketeza vifaa hivi, Biblia na Rozari vimekutwa salama

θ Ni Seminari ndogo ya St. Mary Mbeya
JANUARI 21 mwaka huu zaidi ya  wanafunzi 52 wa Shule ya Seminari ndogo  ya St.Mary’s ya Mbalizi Jimbo Katoliki Mbeya  wamenusurika  kifo kutokana na ajali ya moto ulioteketeza bweni lote na vifaa vilivyokuwemo.  
Aidha  tukio jingine la ajabu ni kutoungua kwa  Biblia  na Rozali Takatifu zilizokuwa zimehifadhiwa katika masanduku ya bati ya wanafunzi  licha ya vingine vyote na jengo kuteketea kwa moto.
 Akizungumza na Gazeti Kiongozi, Gombera wa Seminari hiyo Padri Edwin Mwimba amesema kuwa, tukio hilo limetokea siku ya jumapili mara baada wanafunzi kutoka kanisani majira ya saa 5 asubuhi na kuendelea  na masomo darasani.
Ghafla  wakashtuka kuona moshi ukitokea katika bweni hilo na bahati nzuri hapakuwa na mwanafunzi yeyote aliyekuwepo ndani ya bweni hilo hivyo wote wapo salama.
Padri Mwimba amesema  bado haijafamika kiwango cha athari zilizojitokeza  kutokana na ajali hiyo ambayo pia haijafahamika chanzo licha ya kila kitu kilichokuwepo ndani kuteketea isipokuwa Biblia za wanafunzi pamoja na Rozari Takatifu ambavyo havikuungua.
“Kwa kweli tumekumbana na changamoto  hiyo katika bweni la St. James baada ya wanafunzi kupiga kelele na baadhi ya majirani na wazazi   waliokuwepo jirani walifika tukasaidiana kuuzima moto.
Wakati huohuo tukijaribu kupiga nambari za simu za kikosi cha zimamoto ambazo hazikuwa na majibu hadi tulipowasiliana na Padri aliyekuwepo jimboni ambaye alienda kutoa taarifa kwenye ofisi za zimamomoto  na hatimaye walifika kuuzima ingawa hakuna kitu  tulichookoa, isipokuwa Biblia na Rozari Takatifu,                “amesema.
Gombera huyo ameeleza kuwa bweni hilo  lilikuwa linahifadhi  wanafunzi wa kidato cha kwanza. Baada ya kuteketea lote wamewahamishia katika majengo mengine yaliyokuwepo wazi  na wanaendelea na masomo kama kawaida.
“Kwa ujumla kutakuwepo na uhitaji wa mavazi, magodoro, vitanda, vitabu nk. kwani  wamebakiwa na mavazi waliyokuwa wamevaa  na hiyo ndiyo changamoto  kubwa,” amesema Gombera huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi, Mohamed Mpinga  amethibitisha kutokea kwa tukio hilo  Januari 21 mwaka huu majira ya saa 6.30 mchana  katika shule ya seminari ya St.Mary’s iliyopo Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Nsalala,Tarafa ya Usongwe,Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.
Kamanda Mpinga  amefafanua kuwa bweni moja la St.James  liliwaka moto  na kuteketea lote  pamoja na mali zote za wanafunzi na shule  zilizopo ndani ya bweni hilo, hakuna madhara yeyote yaliyojitokeza kwa binadamu.
Aidha tathmini halisi ya thamani ya uharibifu bado haijafahamika na chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU