Iringa wapata mashemasi 10

Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, Jimbo la Iringa, hivi karibuni ametoa Daraja Takatifu la ushemasi kwa waseminari kumi katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mt. wa Yesu Parokia ya Kihesa.
Waliopata daraja hilo la ushemasi ni Mseminari Alfred Msanzi (Kihesa), Barnabasi Kalinga (Mafinga), Betram Kigodi (Usokami), Eugen Ngatunga (Migoli), Festo Kitosi (Consolata –Mshindo),
 Florence Mlangwa (Ifunda). Jayfa-Zacharia Kayage (Madege), Moses Mgimiloko (Tosamaganga), Nelson Mapembe (Ifunda) na mseminari Polycarp Kindole wa Parokia ya Usokami.
 Askofu Ngalalekumtwa amesema kuwa maaskofu na mapadri wanahitaji wasaidizi ambao ni mashemasi na hatua wanayoindea ina madai makuu ya wema.
 “Maaskofu na mapadri wanahitaji msaada wenu maana tuna kazi nyingi. Mtawasaidia kutangaza neno la Mungu na kutoa sakramenti kadhaa ukiwemo ubatizo, komunyo na ndoa,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa na kuongeza kuwa;
 “Ninyi ni watumishi wa Kristo na Kanisa lake, washiriki na wajenzi wa Kanisa la Mungu, mna vitabu vya sala na muwe na matendo ya uadilifu na wema wenye kujaa roho Mtakatifu na hekima” amesema.
 Amewaambia Mashemasi hao kuwa wamependelewa nafasi hiyo na Kristo hivyo hawapaswi kumuangusha sababu anabaki kuwa mpole na mwema.
 Ameeleza kuwa, Daraja la Takatifu la Ushemasi ni hatua ya mpito, wapo safarini wanapoelekea kwenye ngazi ya ukuhani na hivyo waamini wanapaswa kuwa nao katika sala ili wamalize salama. 
Aidha, kwa nyakati tofauti, Mhashamu Askofu Ngalalekumtwa mwanzoni mwa juma amesali na watoto wa shirika la Utoto Mtakatifu katika Parokia ya Kihesa, huku akiwataka watoto hao kuwaombea viongozi wa serikali ili wawe na haki na watawale kwa amani.
 Ni utaratibu ambao askofu Ngalalekumtwa amejiwekea kusali na watoto kila mwanzoni mwa mwaka na kuwabariki katika masomo yao.
 Mwaka huu watoto hao wamesali kutoka parokia 9 za Vikaria ya Consolata ambayo inahusisha parokia 11 za Jimbo la Iringa.
 “Salini kwa ajili ya wazazi wenu, walezi na walimu wenu, muwaombee pia viongozi wawe na haki na watawale kwa amani, tutunze amani duniani.
 Pia mjifunze mambo mazuri kutoka kwa Yesu ambayo ni wema, upole, ukweli na uaminifu, usafi na matendo mema na unyenyekevu,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU