Ndoa hazijengwi kwa pesa, mali -Ask Kinyaiya
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Beautus Kinyaiya, amesema
baadhi ya wanaume wengi hufikiri na kudhani kwamba kuwa na Pesa nyingi ndio
unaweza kuwa na ndoa imara .
Askofu Kinyaiya amesema hayo hivi karibuni, wakati akitoa homilia
yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya kubariki ndoa tatu na kutoa Sakramenti
Takatifu ya Ubatizo na Kipaimara, katika Parokia ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola
Miyuji Kusini Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Amesema kuwa, kuna wanaume wengi wenye pesa na uwezo mkubwa wa
kiuchumi lakini ndoa zao zimevunjika, hivyo wanapaswa kutambua kwamba ndoa si
kuwa na pesa nyingi bali ni kupendana na kuheshimiana.
“Nahilo wanaume wengi sana huwa wanasahau anafikiri akiwa na hela
sana mwanamke yoyote anaweza kuwa mke wake. Hapana kuna wenyepesa nyingi sana
lakini wameachwa, hawakukubalika au wameachwa.
Pesa sio kila kitu kuna vitu
vya ziada ambavyo anatazama ndani yako anavyoviona na kukubali ulivyo,” amesema
Askofu Kinyaiya.
Aidha amesema kwamba, baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia
dhana ya mwanaume ni kichwa cha familia kuwanyanyasa wake zao, huku akiwataka
wanandoa wote nchini kukiendeleza kile ambacho mke alikipenda kutoka kwa mume
na mume alikipenda kutoka kwa mke wakati wa uchumba wao.
“Kile ambacho mwenzako alikupendea tafadhali endelea kukipalilia,
usiseme ameshanioa kwahiyo basi nakaakaa tu, inaletaga matatizo kwenye ndoa
vile ambavyo vitu alivyovipenda kama havioni tena matatizo yanaanza.
Nawaombeni sana kila mmojawenu kile ambacho mwenzako alikupendea
kishindilie kiendeleze narudia,” amesema Askofu Kinyaiya.
Aidha amewatahadharisha juu lugha wanayoitumia daima ionyeshe
mshikamano na umoja wao kwani kila walichonacho katika familia ni cha kwao wote
na si cha upande mmoja.
Aidha amesema
kuwa, katika maisha ya watu wawili na zaidi kuna mambo ambayo lazima
watakorofishana, hivyo jambo la kwanza
wanalopaswa kufanya ni kupenda kila mmoja kutoa sadaka, huku akisema
wanaume wengi wamekuwa wagumu sana wa kuomba msamaha.
“Na kingine muhimu sana ni kusameheana kwasababu katika maisha
hapa na pale lazima mkorofishane mpo watu wawili na tabia tofauti mahali flani
lazima mtapishana.
Kwahiyo suala la kwanza mpende kila mmoja kutoa sadaka, mambo
flani lazima usamehe, lazima katika maisha ili mwenzako asamehe mambo yaende,”
amesema Askofu Kinyaiya.
Amesema kuwa, wito wa ndoa ni maisha si ya kubadili mke au mume
kama usafiri au kazi, huku akawataka wanandoa kuchunguzana kabla ya
kuandikisha na kufunga ndoa yao, kwani kumekuwa na migogoro mingi inayosababisha
ndoa nyingi kuvunjika.
“hilo ni muhimu sana ndugu zangu na hasa vijana mlioko ndani humu
kwasababu tunaishi karne ambayo watu wanapenda sana wanaishi kitu flani
akikichoka anataka kubadili, mtu ananunua redio akishaichoka leta nyingine, mtu
ananunua bodaboda anakaendesha ikija mpya uza nunua nyingine, hata kazi
tunabadili sana kaa miaka mitano kazini nataka kubadili.
Sasa na mke mnafanya hivohivo hapana, ndoa ni ya maisha na ndiyo maana
huwa tunapenda wanandoa wachunguzane mda wa kutosha,” amesema.
Askofu Mkuu Kinyaiya amehitimisha kwa kuwaasa wanandoa wote
kwamba, mali wanazozipata katika ndoa yao zisiwafanye kutokuelewana bali
waendelee kushikamana hata katika changamoto mbalimbali za maisha.
Misa hiyo takatifu ya kubariki ndoa imeenda sambamba na utoaji wa
sakramenti ya kipaimara kwa wanandoa watatu ambao walikuwa bado hawajaimarishwa
kwa sakramenti hiyo, sanjari na kubatiza watoto wawili Sara na Grece.
Comments
Post a Comment