Askofu Ngalalekumtwa ataka watawa kuiishi Injili
ASKOFU Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa amewataka
watawa kuwa vielelezo vya utakatifu na Injili ili wawe mfano kwa wanadamu.
Askofu Ngalalekumtwa amesema hayo katikati ya juma wakati wa
kuweka nadhiri za kwanza kwa wanovisi 24 wa Shirika la Mtakatifu Teresia Mtoto
Yesu Jimboni humo.
Wanovisi hao wametoka majimbo mbalimbali ya Kanisa
Katoliki nchini na kati yao watatu wametoka nchi ya Haiti.
Misa hiyo imefanyika kwenye kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu
Parokia ya Tosamaganga na kuhudhuriwa na mapadri, watawa wa kike na kiume
pamoja na waamini wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki
Iringa.
Askofu Ngalalekumtwa amesema kwamba ikiwa watawa hao watakuwa ni
vielelezo vizuri watawashawishi na wengine kuiga maisha yoa.
Amesema kuwa, wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na anawaombea ili
waweze kuzingatia ukweli wa majitoleo yao.
“Tunawaombea Kristo na Mama Bikira Maria aliye mfano wa mabikira,
na Mtakatifu Teresia aliyemsimamizi wenu awasimamie katika utume wenu” amesema
askofu Ngalalekumtwa.
Aidha askofu Ngalalekumtwa amesema kuwa, popote pale Kanisa
litakapowahitaji sehemu yoyote wapate kuenenda vile Kristo anavyotaka.
Askofu Ngalalekumtwa amewataka pia waamini wote kuwaombea watawa
hao, na pia watambue kwamba wanahitaji upendo wao, sala zao ili waweze kuviishi
viapo vyao kwa uaminifu.
“Kumfausa Kristo ni kazi ngumu yataka Neema ya Mungu, likiwepo
Kanisa, shirika na Ulimwengu wahitaji watawa wenye msimamo unaoleweka,”
amesema.
Comments
Post a Comment