Uhai wa Kanisa si wingi wa mapadri, waamini, watawa
Askofu
wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi Mhashamu Askofu Filbert Felician Mhasi
amewakumbusha waamini kuwa uhai wa Kanisa siyo wingi wa waamini makanisani,
waseminaristi maseminarini, watawa katika nyumba za kitawa bali ni maisha yao
ya Imani wanayoyaishi.
Rai
hiyo ameitoa hivi karibuni akiongoza
Misa Takatifu katika Seminari Kuu ya
Mtakatifu Paulo Mtume Kipalapala Tabora akitoa huduma ya usomaji Masomo
kanisani na huduma altareni kwa mafrateri wa mwaka wa pili na watatu.
Askofu
huyo amesema uhai wa Kanisa hautegemei wingi wa mafrateri katika seminari na
swali muhimu ni Je, wanastahili?
Aidha
Askofu Mhasi amesema Upadri unajengwa katika maisha imara ya Ukristo, tunakuwa
wakristo kabla ya kuwa mapadri hivyo ni wajibu
wa kila mkristo kuishi imani yake kwa uaminifu. Amewakumbusha mafrateri
hao kuwa mabalozi kule waendako baada ya kuwa mapadri.
Maisha
ya Upadri ni sawa na mbio za kijiti, watu tunapasiana kila mmoja kwa wakati
wake na stamina yake, ni vema zamu yako ikifika ukimbie haraka ili Injili isije
ikafia mikononi mwako, tumia karama zako na nguvu zako kukimbiza Injili ya
Kristo kwa haraka.
Kila
Mseminaristi anapaswa kujivunia nafasi ya kwanza ya kuwa mkristo na kuishi
Ukristo, “mafrateri jiepusheni na tamaa ya vyeo kanisani, ridhika na nafasi ya
kwanza ya kuwa mbatizwa uwe mkristo na uishi ukristo, ndiyo upadri na Uaskofu
utafuata.
Acheni kujiwekea matarajio makubwa kanisani
mtaishia kuchanganyikiwa bure,” Askofu amesema.
Aidha
Askofu Mhasi amesema mara baada ya Kristo Yesu kumaliza utume wake wa kimwili
duniani aliacha sera ya kwenda kuhubiri Injili ulimwenguni pote mpaka ukamilifu
wa dahari, hiyo ndiyo kazi ya upadri mnayoiendea, nendeni mkawe alama ya uwepo
wa Mungu ndani yenu.
Amesema
waseminaristi hawana budi kuwa wasikifu kwa walezi wao ili baada ya malezi wawe
mapadri wema na watakatifu.
Mseminaristi
au frateri hapaswi kuwa na haraka ya kupewa daraja ya upadri, vyote hutolewa na
Mungu kwa wakati anaoona unafaa.
Aidha
Askofu huyo amesema Mungu ndiye anayeita, anayechagua kuwa chombo chake kwa
wakati wake, katika mazingira anayotaka yeye , hata kwa macho yetu ya
kibinadamu kama tunayaona hovyo, akitaja wito na tabia ya Mtume Paulo aliyekuwa
na kibali cha kuua lakini Mungu alimwita na kumtumia.
Mwisho
Askofu Mhasi amewaasa mafrateri wote kutumia muda wao vizuri wawapo seminarini
ili baada ya malezi wakawe wahudumu wazuri na bora wa Kristo na si bora mapadri
na kuwaomba wakae mbali na tamaa ya vitu na malimwengu.
Comments
Post a Comment