Askofu Amani awapongeza watawa wa Shirika jipya Arusha walioweka nadhiri
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mha.
Isaac Amani, ameitaka jamii kuwa tayari na kufanya maandalizi ya kina katika kuitikia
na kuuchuchumilia wito wowote wa maisha wa kuwatumikia watu kadri ya mpango
wake Mungu Mwenyezi.
Rai hiyo ameitoa mwishoni
mwa wiki jimboni humo akiihubiria hadhira ya waamini waliofurika katika Kanisa
la Mt. Yokobo Mtume Parokiani Moshono kwenye sherehe za kuweka nadhiri za
kwanza za kitawa kwa masista watatu wa kwanza wa Shirika jipya la Kimisionari
la Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya.
Askofu Mkuu Amani
amefafanua kuwa wito uwe wa maisha mathalani;
ndoa, utawa na upadri au wa kitaaluma na wa kiuongozi chimbuko lake ni
Mwenyezi Mungu mweyewe anaeanzisha na kumwita mtu kutumika ipasavyo na wala si
kutumikiwa. “Mwenye kuita ni Mungu na mwenye kuitwa ana kazi tatu kuu, mosi
kuisikia sauti ya Mungu, pili kuitikia kwa kuikubali na kuishi agizo la Mungu
na tatu ni kufikisha ujumbe wa Mungu kwa
watu kwa ajili ya maendeleo yao ya kiroho, kimwili na kijamii”, amesema Askofu Mkuu Isaac Amani.
Akiwapongeza na kuwaasa
masista watatu walioweka nadhiri hizo za kwanza za maisha ya kitawa ambazo ni
usafi wa moyo, ufukara na utii, Askofu Mkuu Amani amesema, “ Wanangu Masista
Dafrosa Neema Shayo kutoka Jimbo la Moshi, Daria Markus Ndaligwa kutoka Jimbo
la Iringa na Monika Godfrey Mdoe kutoka Jimbo la Tanga, nawapongeza sana kwa
kuitikia wito huu wa kuwa wachumba wa Bwana wetu Yesu Kristo, nawasihi sana
msiangalie nyuma na kuwaza habari ya kuchagua wito mwingine, endeleni kuisikia
sauti yake Kristo ndani yenu, mkiishi kiaminifu nadhiri zenu katika kumtumikia
Mungu na watu wake, na sanjari na hilo nawapongeza pia wazazi kwa kuwatoa
watoto wenu kwa Kanisa, sasa wasaidieni na wala msiwe kikwaza kwao mathalan
kuanza kuwaomba wawasaidie kiuchumi au kuwatafutia ufadhili wa kusomesha wadogo
zao.”
Kwa upande wa mwanzilishi
wa Shirika la Masista Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya Sr.
Gisela Upendo, akionesha furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu amesema, “
hakika kwa unyenyekevu mkubwa namtukuza Mungu nikijawa shukrani za dhati kwake
na kwa Uongozi Hairakia wa Kanisa letu, Serekali ya Nchi yetu, sanjari na watu mbalimbali ambao kwa sala, nia
njema, shime na misaada mbalimbali leo hii tunashuhudia matendo haya makuu ya
Mungu, kwao wote, tunawaahidi sala zetu kwani hatuna zaidi cha kuwapa.”
Mbali na utume wa
kufundisha dini mashuleni, kutembelea wagonjwa na kushiriki sala za Jumuiya
Ndogo Ndogo, Shirika hili changa kabisa jimboni Arusha, kwa kipindi kifupi cha
takribani miaka mitano tangu kuanziswa kwake, kupitia wafadhili kutoka Bolzano
Italia limefanikiwa kujibu kero ya jamii ya maji safi na salama kwa kuchimba na
kusambaza maji ya kisima kwa shule nne za serikali na kwa jamii kubwa ya Kata
ya Baraa Moshono.
Na kwa sasa Shirika hilo
kupitia ufadhili kutoka taasisi ya Circle Association for Cooperation and
Development linajenga chuo cha ufundi
mbalimbali kwa ajili ya vijana wa familia masikini ili kuwawezesha kujiajiri mara
baada ya kufuzu masomo yao. Ujenzi huo kwa sasa umefikia hatua ya lenta na
ukikamilika chuo kitakuwa na uwezo wa kuwa na vijana mia mbili.
Shirika la Masista
Wamisionari wa Ekaristi Takatifu na Uinjilishaji Mpya lilianzishwa Jimboni
Arusha kwa ruhusa ya Askofu Mstaafu
Josaphat Lebulu baada ya taratibu zote za Kikanisa kukamilika huko Roma Italia
na limesajiliwa na Serikali Nchini. Kwa sasa chini ya uongozi wa Mwanzilishi wake
ambae ni Mtanzania wa kutoka Jimbo Katoliki Same Sr. Gisela Upendo, shirika
lina idadi ya walelewa 23,Wanovis 3,Wapostolant 7,Wakandidat 13 na masista 3 ambao mwishoni mwa wiki waliweka
nadhiri zao za kwanza na kufikisha idadi ya Masister kuwa 4.
Comments
Post a Comment