Picha zenye maudhui ya ngono kichocheo maambukizi ya ukimwi

Wazee Wilayani Kondoa wameiomba Serikali kudhibiti picha zenye maudhui ya ngono katika mitandao ya Kijamii kwa lengo la kusaidia kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI.
Wamesema picha hizo zisizo kuwa na maadili zinawachochea vijana  kujiingiza katika matendo yanayosababisha maambukizi ya UKIMWI.
Wazee hao wameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wazee wa mila pamoja na viongozi wa dini yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwafundisha kuhusu  ukubwa watatizo la UKIMWI kwa vijana na kuwataka kusaidia kupambana na tatizo hilo katika jamii kupitia nafasi zao.
Mzee Mohamed Hussein Kola akitoa maoni yake katika kikao hicho amesema hata siku mmoja hakuna mtu aliyefikishwa mbele ya sheria kwa kuambukiza mwenzake ukimwi kwa makusudi pamoja na uwepo wa sheria ya ukimwi hapa Nchini.
Mzee Kola ameangazia pia suala la malezi na kusema kwamba vijana hawaheshimu tena mawazo ya wazee na kudai kuwa kila mzee akitoa maoni yake vijana wanasema mawazo ya mzee nayo yamepitwa na wakati na kudai kuwa hata kwa baadhi ya mafunzo ya magonjwa mbalimbali yanapotolewa wazee wamekuwa hawashirikishwi.
Mzee Haruna Ramadhani Dodi pia ameongeza kuwa vijana wadanganyana kupuuza uwepo wa maambukizi ya ukimwi na kudai kuwa watakufa kishujaa huku akiwataka kupuuza mawazo hayo kwani hakuna mtu aliyewahi kufa kishujaa.
 Pia ametahadharisha jamii na serikali juu ya uwepo wa maeneo ya biashara za kumbi za starehe kuwa zinachangia uwepo wa maambukizi. 
Taarifa hizi kwa wazee hao zilikuwa za kushtua kwani idadi ya maambukizi ya ukimwi kwa vijana inazidi kupaa na hii imeelezwa na Afisa Maendeleo Mkuu kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Matias Haule aliyesema kuwa watanzania 200 wanapata maambukizi mapya ya ukimwi kwa siku.
Aidha Bwana Haule ametoa takwimu hizo na kuongeza kuwa maambukizi haya kwa mwaka ni kiasi cha watu elfu 72 akiitaja idadi ya watu inayoambukizwa kwa mwezi kuwa watu elfu 6,000 na kushangaza wazee hao kwa kusema kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 maambukizi mapya kwao 79 na kati yao wasichana wanaombukizwa ni 63 hivyo idadi kubwa ya wasichana inaambukizwa ukilinganisha na wavulana.
Wizara ya Afya Maendealeo ya Jamii kwa Kushirikiana na TACAIDS pamoja na Shirika la TASAF wako Mkoani Dodoma kutembelea wasichana na wanawake vijana pamoja na Shule mbalimbali Mkoani humo kwa lengo la kuhamasisha vijana juu ya tishio jipya la maambukizi ya ukimwi kwa vijana na zoezi hilo litaendelea kwa Mkoa wa Morogoro na baadae nchi nzima.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI