Serikali yashangazwa na uwezo wa Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu
MAONESHO ya miradi bunifu ya wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yosefu Tanzania, wa Uhandisi, Ualimu wa Sayansi na
Hisabati, na Udaktari wa Binadamu yanayofanyika Agosti 29 hadi 31, 2018 ndani
ya viwanja vya Mlimani City yameifanya serikali ikiri kuwa kiwango kikubwa cha
elimu inayotolewa na chuo hicho itasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika
jamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri,
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa
maonesho hayo, na kusema kuwa vijana hao watasaidia kukuza falsafa ya serikali
ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda.
“Kwanza kabisa nataka nikiri
kwamba leo ndio nimeona kwa kiwango kikubwa elimu inayokwenda kumsaidia
mtanzania kutatua matatizo mbalimbali katika jamii. Nimefurahi sana kuwaona vijana wa kitanzania
wanachuo wakionyesha uwezo wa juu kabisa kuja na utatuzi mbalimbali wa matatizo
tuliyonayo na namna bora ya kuweza kuyakabili matatizo hayo” amesema.
Aidha ameeleza kuwa maonesho hayo
yanampa ujasiri kwamba nchi itapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwatumia
wataalamu wa ndani, kikubwa wanachohitaji ni uwezeshwaji.
“Huwa najisikia vibaya sana
kusikia tunawasifia vijana wa nchi jirani kwamba wana uwezo mkubwa. Vijana wa
kitanzania mna uwezo mkubwa sana wa kwenda kushiriki kwenye ustawi wa Taifa
letu na kuikuza Tanzania hasa katika falsafa ya serikali ya awamu ya tano ya
serikali ya viwanda. Pongezi kwa Chuo cha Mtakatifu Yosefu, nilikuwa napita
pale barabarani nakiona lakini sikujua kama mko organized kwa namna niliyoiona
leo” ameongeza.
Pia Mavunde amebainisha kuwa
ubunifu huo ni namna kubwa ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano
ya serikali ya viwanda, kwa kuwaanda wataalamu ambao watasaidia nchi kupiga
hatua.
“Kazi kubwa za kiubunifu
zinakwenda kutatua changamoto mbalimbali. Kama nchi tukitumia wataalamu hawa wa
ndani tutapunguza gharama za uendeshaji. Tukiwatumia vizuri wataalamu wetu wa
ndani Taifa litapiga hatua mara dufu. Nimeona mifumo mbalimbali hapa kama ile
ya kupunguza ajali, kilimo, ukusanyaji wa mapato nk” ameeleza.
Katika hatua nyingine Mavunde
amevutiwa na ubunifu wa msichana mmoja ambaye amebuni teknolojia rahisi
inayosaidia katika uhifadhi wa mafaili, na kuahidi kumpeleka binti huyo kwa
waziri anayeshugulikia masuala ya Utumishi wa Umma.
“Moja kati ya changamoto
tuliyonayo katika mifumo yetu ni pamoja na mfumo wa handling ya mafaili. Mengi
hupotea, utafutaji wake hufanywa manually na huchukua muda mrefu, lakini leo
kupitia wanachuo hawa wanakuja na suluhisho ambalo halina gharama kubwa. Na
kama nilivyoahidi nataka nimchukue yule binti nimpeleke kwa waziri wa
Utumishi Mheshimiwa Mkuchika akae kwa
dakika chache tu amsikilize alichonacho” amebainisha.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa
Chuo hicho Prof. Burton Mwamila amesema kuwa wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo
wana uwezo mzuri wa kuweza kuchangia katika ajenda ya Tanzania ya viwanda,
kinachohitajika ni mazingira wezeshi ili ule ubunifu wanaouonyesha wakiwa
chuoni uweze kuendelezwa.
“Tuweke mikakati ya kuwawezesha
hawa vijana kwa kuwa miradi mingi bunifu iliyoonyeshwa hapa inaweza ikageuzwa
ikawa viwanda” amesema.
Comments
Post a Comment