Msimamo wa Magufuli kuhusu uzazi wa mpango wapongezwa
MSIMAMO
alioutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli juu
ya uzazi wa mpango umepongezwa kwa kuwa kukithiri kwa vitendo vya matumizi ya
vidhibiti mimba kumeharibu taifa na kushambulia maadili, utamaduni na imani ya
taifa huku dhana hizo zikiwa ni itikadi ovu za magharibi za kudhibiti ukuaji wa
idadi ya watu.
Pongezi hizo zimetolewa na
Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Uhai nchini (Pro life) Emil Hagamu katika
tathmini yake ambapo amesema kuwa watu wa Ulaya wamepita katika miongo
mbalimbali, imefikia mahali wameharibikiwa hivyo mawazo na itikadi zao ovu
ndizo zinazoletwa kwetu Afrika hasa Tanzania.
“Hiki ndicho Nyerere alichosema,
alisema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Kwa
hiyo watu ndiyo namba moja. Asikudanganye mtu, nchi zote za Ulaya zilipata
maendeleo kwa sababu kuu tatu: Walitunyonya kiuchumi na kisiasa, biashara ya
utumwa ambapo walihitaji watu, na idadi yao ni kubwa. Uki promote
contraceptives na abortion utasababisha idadi ya watu kupungua, na ikipungua
kila kitu kinarudi nyuma” ameeleza Hagamu.
Aidha Hagamu ameweka wazi kuwa
watu wa magharibi wanaokuja kuhamasisha matumizi ya vidhibiti mimba
wanakabiliwa na upungufu wa idadi ya watu katika nchi zao ambako kwa sasa wanahamasisha watu kuzaa na wamefungua
milango kwa wahamiaji ili idadi ya watu isipungue sana.
“Tunamuunga mkono Rais na tunampa
hongera na tunaomba aseme zaidi kwa sababu hawa mabeberu wanaotaka kutumaliza
hawana nia njema. Sasa hawa kule kwao wanahamasisha kuzaa halafu wanakuja huku
kwetu wanakuja kupunguza vizazi sasa huoni huu ni uendawazimu?” amehoji.
Msimamo wa Rais Magufuli
Akizungumza na wanachi wa Wilaya
ya Meatu mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara, Rais Magufuli amesema kuwa
hakubaliani na kampeni za uzazi wa mpango na kuwataka wanachi wafanye kazi na
wakiwa na chakula cha kutosha wazae ili nguvu kazi ya taifa iimarike.
“Najua waziri hapa anapenda
kuzungumzia uzazi wa mpango, na ndio maana mimi mambo mengine huwa sikubaliani
nao. Ziko nchi zilipangiwa mpango wa kuzaa leo wanajuta wanatafuta mtu wa kuzaa
katika nchi zao. Mimi nawaeleza ukweli, mtadanganyika kwa mipango mingine ya
ajabu sana. Tunachotakiwa watanzania tuko milioni 55 ni kuchapa kazi ili kusudi
utakaowazaa uwalishe. Kama huwezi kufanya kazi hapo ndipo uende kwenye mipango
ya uzazi” ameeleza Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameongeza
kuwa “Mimi ninachowaomba ndugu zangu mbele ya Waziri wa Afya ambaye anaongea
mambo ya ku control uzazi, limeni, fanyeni kazi, ukiwa na chakula cha kutosha
zaa. Watu wameshaingiwa na mawazo ya ajabu katika nchi”.
Kanisa linasemaje?
Mwaka 1968, Baba Mtakatifu Paulo
VI aliandika insiklika iitwayo ‘Humanae Vitae’
ikijibu kiu ya watu ndani ya kanisa, mintarafu matumizi ya vidhibiti
mimba, kama ni vyema ama si vyema kutumia vidhibiti mimba, na kuainisha njia bora
za kupanga uzazi kwa njia ya maumbile kama Mungu alivyoratibisha.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa mnamo
mwaka 1930, Umoja wa Makanisa ya Kianglikana katika mkutano wao wa Lamberth,
ingawa walikubali kuwa, njia bora ya kupanga uzazi ni ile itumiayo mwenendo wa
maumbile, lakini waliruhusu matumizi ya vidhibiti mimba kwa wanandoa wenye
matatizo ya pekee.
Ruhusa hii ilifungua milango kwa
matumizi ya vidhibiti mimba hata pasipo matatizo yoyote, na hatimaye ukawa ndio
mtindo wa kupanga uzazi kwa watu wa ndoa.
Kutokana na ruhusa hiyo ya
Waanglikana na kutokana na kuongezeka kwa vitisho dhidi ya taasisi ya ndoa,
Baba Mtakatifu Pius XI, mnamo Decemba 31, 1930 alitoa tamko la Kanisa Katoliki
kuhusu matumizi ya vidhibiti mimba.
“Kwa sababu yoyote, hata kama ni
kubwa kiasi gani, haitaruhusiwa matumizi ya njia ambazo kwa asili yake ni ovu
dhidi ya maumbile na kuzifanya zikubalike kimaadili kama vile zingekuwa njema.
Kwa vile tendo la ndoa limeelekezwa kimaumbile katika uzao wa watoto, wale
wanaoliharibu kwa makusudi na kuliondolea uwezo wake wanatenda dhambi dhidi ya
maumbile na wanajiletea aibu na uovu wa ndani. (Casti Cannubii, Na 54)”
Comments
Post a Comment