Hii ndiyo nguvu ya Kanisa Katoliki Tz
Likiwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka
150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Kanisa Katoliki nchini limeendelea kuwa
kielelezo katika utoaji wa huduma za elimu, afya na za kijamii bila upendeleo
hasa kwa watanzania wanaoishi maeneo ya vijijini.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande amesema kuwa Kanisa litaendelea kutoa
huduma za afya na elimu nchini kwa kufuata yale yaliyofanywa na Kristo, ambaye
alitibu na kufundisha.
“Endeleeni kushiriki kikamilifu, shirikishaneni mang’amuzi yenu katika
utoaji huduma ili kuwafanya wale tunaowahudumia waone kuwa ufalme wa Mungu
umetamalaki” ameeleza Askofu Nkwande ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Afya
TEC.
Aidha Askofu Nkwande ametoa rai kwa wajumbe wa mkutano huo kujikita
katika kufanya utafiti, uvumbuzi na mafunzo badala ya kujikita katika kutibu
peke yake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TEC Padri Dkt. Charles Kitima amesema
kuwa utoaji wa huduma za afya ni kiini cha utume wa Kristo na Kanisa, ambapo
amewataka wajumbe wa mkutano huo ambao ni Wakuu wa Idara za Afya katika majimbo
Katoliki nchini na watawala katika Hospitali za Kanisa, kuendelea kutoa huduma
za afya kwa weledi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanawaponya watu siyo tu
kimwili, pia na kiroho.
“Utoaji wa huduma za afya ni moja kati ya malengo ya Kristo na Kanisa.
Katika utoaji wa huduma hizo tunamtibu mwanadamu kimwili na kiroho pia,
tuendelee kutoa huduma hizo bila upendeleo huku tukigusa maisha ya kila mwenye
uhitaji” ameeleza.
Serikali yaomba Kanisa liwekeze kwenye viwanda
Akitoa neno kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zuhura Mguni amesema kuwa serikali inatambua
mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma za afya nchini tangu
ujio wa wamisionari wa kwanza waliotokea Zanzibar hadi Bagamoyo.
Ameliomba Kanisa kuwekeza kwenye viwanda kadiri ya huduma mbalimbali
ambazo Kanisa inazitoa kwa watanzania ili kuendana na azma ya Serikali ya awamu
ya tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda.
“Serikali inatambua kazi ya ukarimu ambayo Kanisa inafanya kwa
watanzania. Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa katika kuwahudumia
watanzania” ameeleza.
Idadi ya hospitali, vituo vya afya na shule za Kanisa hii hapa
Akielezea hali halisi ya utoaji huduma za afya unaofanywa na Kanisa
Katoliki nchini Katibu wa Idara ya Afya TEC Jovin Riziki amesema kuwa Kanisa
lina jumla ya hospitali 55, vituo vya afya 93 na zahanati 335 huku likichangia
asilimia 32 ya huduma za afya kwa Taifa. Jumla ya sehemu (facilities) ambazo
kanisa linatoa huduma za afya ni 483.
Kwa idadi hiyo, takribani kila wilaya nchini inapatiwa huduma za afya na
Kanisa Katoliki, huku taarifa zaidi zikibainisha kuwa huduma hizo zinatolewa
zaidi maeneo ya vijijini ambako kuna uhitaji mkubwa.
“Idara za afya ipo chini ya Kurugenzi ya Huduma za Jamii ambayo
inajumuisha Idara ya Afya na Elimu. Utoaji wa huduma za jamii unaofanywa na
Kanisa Katoliki nchini Tanzania hutimiza huduma ya Uponyaji na Kufundisha ya
Bwana wetu Yesu Kristo kwa watu wote” ameeleza Riziki.
Miongoni mwa Hospitali 55, hospitali moja ni ya Kanda ambayo ni
Hospitali ya Bugando (Kanda ya ziwa), hospitali 6 za rufaa kwa ngazi ya mkoa,
na hospitali 19 za miji.
Wakati huo huo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu wa Idara ya
Elimu TEC Padri Alphonse Raraiya, inaelezwa kuwa Kanisa Katoliki nchini lina
jumla ya shule za msingi 100, Shule za Sekondari na Seminari Ndogo 235, vyuo
vya ufundi 75, vyuo vikuu 4 na kila jimbo likiwa na shule za awali.
Jumla ya taasisi zote za utoaji wa elimu zinazoendeshwa na kumilikiwa na
Kanisa Katoliki nchini ni zaidi ya 500.
Comments
Post a Comment