Ask. Ngalalekumtwa aadhimisha Yubilei miaka 25 na kupadrisha mashemasi 13
ASKOFU wa Jimbo
Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa hivi karibuni ameadhimisha
Yubilei ya miaka 25 ya uchungaji jimboni Iringa na katika maadhimisho hayo
ametoa Daraja Takatifu ya Upadri kwa mashemasi 13.
Maadhimisho
hayo yamefanyika katika viwanja vya kichangani na mara ya kwanza kwa jimbo hilo
kupata idiadi kubwa ya mashemasi na
hivyo kuliweka katika historia.
Misa
Takatifu ambayo imeongozwa na Askofu Mkuu Damian Dallu wa Jimbo Kuu Katoliki
Songea na homilia kutolewa na Askofu Ngalalekumtwa imehudhuriwa na zaidi ya
mapadri 100 kutoka ndani na nje ya jimbo la Iringa, watawa wa kike na kiume
pamoja waamini kutoka sehemu mbalimbali za jimbo la Iringa
Akitoa
homilia kwenye maadhimisho hayo, Askofu Ngalalekumtwa amewataka mapadri hao
wapya wawe faraja, sala, huruma wapole wema na pia wawe waaminifu kwa viapo
vyao.
“Jitahidini
kuishi maisha ya kiinjili yaani ya baraka ili watu wampate Kristo ndani yao na
pia waiendeleze kazi ya uinjilishaji, watambue kwamba wazazi wao wamewatoa kwa
kanisa na kamwe wasirudi nyuma na wajue kwamba wao ni wajumbe wa habari njema”
amesema.
Awali kabla ya kuanza kwa misa hiyo Takatifu,
Makamu wa Askofu Jimbo la Iringa Padri Vincet Mwagala ambaye pia ni Paroko wa
Parokia ya Ifunda, amesema kwamba wanamshukuru Mungu kwa sababu miaka 25
iliyopita wana Iringa walipewa zawadi ya Kuhani, Mchungaji Mkuu wa Jimbo,
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa.
“Tunakushukuru
wewe mwenyewe kwa kutii sauti ya Mungu, na hivi kututumikia kwa miaka hii 25,
tunakuombea ili Mwenyezi Mungu aendelee kukujalia afya njema ya mwili na Roho.
Baba, wewe umekuwa mtumishi wa wote, ndiyo maana leo tupo hapa wakristo na
wasio wakristo kumtukuza Mungu kwa upendo wake ambao umekuwa ukidhihirika
kupitia wewe mtumishi wake” amesema.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyoandikwa na Padri Marko Kihwelo kwa niaba ya kamati ya Liturujia
Jimbo, imesema kuwa tarehe 06.01.1988 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alimteua
Padri Tarcisius Ngalalekumtwa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo la Sumbawanga
ambako alijitoa mhanga katika kulitumikia taifa la Mungu kwa juhudi.
Askofu
Ngalalekumtwa alihamishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kutoka jimbo la
Sumbawanga na kuwa askofu wa Iringa na tarehe 10.01.1993 alisimikwa rasmi kuwa
Askofu wa jimbo la Iringa kushika nafasi ya Askofu Norbert Mtega ambaye
alihamishiwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea.
Tangu
kuingia kwake jimboni Iringa, parokia kadhaa zimeongezwa ambazo ni Migoli,
Mtandika, Madege, Nyololo, Ipogolo, Kidamali, Parokiaya vyuo vikuu, Mapanda na
Mbarali, mpaka sasa Jimbo la Iringa lina jumla ya parokia 38.
Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa alizaliwa tarehe 25.10.1948 katika kijiji cha Banavanu
Parokia ya Tosamaganga Mkoa wa Iringa kwa wazazi Joseph Ngalalekumtwa na Mama
Magdalena Sekutika. Alibatizwa Parokiani Tosamaganga tarehe 15.11.1956 na
kupewa sakramenti ya kipaimara siku hiyo hiyo na mhashamu Askofu Attilio
Beltramino, I.M.C, na komumyo ya kwanza.
Mwaka 1956 alianza masomo ya elimu ya msingi
katika shule ya msingi wavulana Tosamaganga ambayo kwa sasa inaitwa shule ya
msingi Lupalama A hadi mwaka 1959. Mwaka uliofuta alijiunga na seminari ndogo
ya Tosamaganga ambapo alisoma hadi mwaka 1967. Akiwa na wito wa kumtumikia Mungu katika upadri,
aliamua kuendelea na masomo ya seminari, mwaka 1968 alitumwa seminarini Kuu ya
Peramiho kujiunga na masomo ya Falsafa.
Mwaka 1969 alitumwa Roma, Italia, kusomea
Teolojia katika Chuo Kikuu cha Propaganda Fide. Alisoma chuoni hapo hadi mwaka 1974 alipohitimu masomo yake vizuri na
kujipatia shahada katika fani ya Elimu Mungu ( Lincence in Dogmatics). Tarehe
07/04/1973 alipata Daraja Takatifu ya Upadri huko San Ginesio, Camerino, Italia
alipewa na Askofu Bruno Frattegiani.
Akiwa padri
tayari alirudi nchini Tanzania Oktoba 1974. Askofu Mario Mgulunde alimtuma
Padri Ngalalekumtwa parokini Ifunda, huko alifanya utume kuanzia tarehe
18/11/1974 hadi tarehe 05/12/1976.
Mwaka 1977
alitumwa na Askofu Mario Mgulunde Seminari Kuu Peramiho kuwa mkufunzi na mlezi,
kwa unyenyekevu alipokea utume huo. Haukupita muda mrefu, akateuliwa kuwa
Gombera wa Seminari kuu ya Paremiho, akishika nafasi iliyoachwa wazi na
mtangulizi wake Padri Emmanueli Mapunda, ambaye alitumwa Roma kwa masomo. Padri
Ngalalekumtwa aliongoza seminari hiyo hadi tarehe 30.03.1982. bTarehe
11.04.1982, alitumwa seminari ndogo ya Mafinga kuwa Gombera hadi Desemba 1988.
Comments
Post a Comment