Mpeni Mungu nafasi ya kwanza-Ask. Ruwa’ichi
WAKRISTO wakatoliki nchini wameaswa kumpa Mungu nafasi
ya kwanza kwa kuwa hakuna anayejua siku wala saa atakayoitwa na Mungu.
Wito huo umetolewa na Askofu
Mkuu Yuda Thadei Ruwa’ichi wakati wa homilia yake kwenye adhimisho la ibada
maalumu ya Misa Takatifu ya kumuombea marehemu Askofu Mstaafu Nestor Timanywa
wa Jimbo Katoliki Bukoba aliyefariki Agosti 28, 2018 katika Hospitali ya Rufaa
ya Bugando.
Askofu Ruwa’ichi amesema kuwa
Yesu anawaasa waamini wawe tayari na wito wa kuwa tayari unapaswa kupokelewa
kwa uzito mkubwa. Ameongeza kuwa mara nyingi mwanadamu anapokuwa na afya nzuri
anasahau kuwa kuna kifo na kuwa anapaswa kutoa hesabu kwa Mungu kwa kuwa uhai
siyo mali ya binadamu, bali ni mali ya Mungu.
Amebainisha kuwa Mungu ndiye
aliye hai, na uhai kwake siyo kitu cha kupewa na uhai ni hulka yake na kwamba
binadamu wapo hai kwa sababu ya huruma yake na kwa kutambua hilo ni muhimu
kumpa Mungu nafasi ya kwanza, kila dakika ya maisha ya kila mmoja.
Adhimisho hilo maalumu la
kumwombea Marehemu Askofu Timanywa lililofanyika katika Kanisa Kuu la Epifania
Bugando, liliongozwa na Askofu Mkuu Ruwa’ichi na lilihudhuriwa na Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya na Askofu wa Jimbo
Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala.
Comments
Post a Comment