Niko tayari kuwatumikia -Ask. Ruwaich

+ Kard. Pengo aeleza sababu za kuomba mwandamizi 
Na Na Pascal Mwanache, Dar es salaam
ASKOFU Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaich amesema kuwa amepokea kwa shukrani uteuzi wake na kuwaeleza waamini wa jimbo hilo kuwa yuko tayari kuwatumikia kwa utii licha ya changamoto za mazingira mapya ambazo huenda atakutana nazo.
Ameeleza hayo katika Misa Takatifu ya kupokelewa kwake jimboni Dar es salaam, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Septemba 7, 2018 na kuhudhuriwa na mamia ya waamini wa jimbo hilo.
“Napokea yote kwa shukrani nikijiaminisha mikononi mwa Mungu. Ninayo nia thabiti ya kushirikiana nanyi katika kulihudumia taifa la Mungu, kwani katika Kanisa huwa hakuna kuhama; kuna kutumwa na kutumikia. Niko tayari kuwatumikia” ameeleza Askofu Ruwaich.
Aidha Askofu Ruwaich ameahidi kuwaombea wana Jimbo Kuu Katoliki Mwanza wanapoingia katika kipindi kipya cha kuwa katika jimbo lisilokuwa na mchungaji mkuu, ili wapate askofu huku akiwaasa daima wamtumainie Mungu.
“Mpokeeni Kristo ndiye mchungaji wetu, yeye hahami wala hahamishwi, msiache kumtumainia yeye” ameeleza.
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amempongeza Askofu Ruwaich kwa utii na uthubutu wa kupokea utume aliopewa na Baba Mtakatifu Fransisko  licha ya uzito wa utume huo.
Aidha amempongeza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kuwezesha mchakato wa kumpata mapema mwandamizi wake, kwa ushirikiano na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa, mapadri na waamini.
“Tunakupongeza kwa utii na uthubutu wa kupokea utume uliopewa na Papa licha ya uzito wa kazi inayokukabili katika utume mpya hapa Dar es salaam ambapo kuna idadi kubwa ya watu, wingi wa shughuli za serikali na za kimataifa, mambo ambayo yanadokeza utofauti kati ya Mwanza na Dar es salaam” amesema Askofu Nyaisonga.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameeleza kuwa ni yeye mwenyewe ndiye aliyemuomba Baba Mtakatifu Fransisko ampatie askofu mwandamizi, na amempongeza Askofu Ruwaich kwa kukubali kupokea utume huo.
“Ni mimi mwenyewe niliyemuomba Papa anipatie mwandamizi. Halikuwa neno dogo kwake kukubali kuja Dar es salaam, kwa hivi ninampongeza sana” ameeleza Kardinali Pengo.
Aidha amewaambia waamini wa jimbo hilo kuwa bado ataendelea kuwepo Dar es salaam na hata baada ya kukabidhi ofisi kwa askofu mwandamizi ataendelea kuwa miongoni mwao.
“Kwa miaka 28 mlinitunza kama askofu, hata nikikabidhi kwa askofu mwandamizi nitakwenda wapi? Nitakuwa  hapa hapa Dar es salaam” ameeleza Kardinali Pengo huku akishangiiwa na waamini waliokusanyika katika viwanja vya kanisa hilo.
Katika homilia yake Kardinali Pengo amewaasa waamini kulitambua na kulikubali fumbo la umwilisho, na kufanya kila kitu pamoja na Kristo na kwa niaba yake.
“Sisi ni wainjilishaji wa ngazi ya juu katika Dar es salaam. Mtuombee tuwe na imani ya kutambua kuwa Yesu ni mwokozi wa ulimwengu, Yeye ni Mungu na mwanadamu. Tuwaombee waamini wawe tayari kutusikiliza tunapotangaza ukuu wa fumbo hili la umwilisho” ameeleza.
Katika hatua nyingine Kardinali Pengo amegawa majukumu mapya ya kitume katika jimbo hilo huku akimpatia Askofu Ruwaich kusimamia idara za Uchungaji, Utume wa walei, Teolojia, Utume wa familia, Haki na amani, Eukumene na Caritas.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU