Kanisa laondokewa na watumishi watano ndani ya siku 7
KANISA Katoliki nchini limepata pigo mara baada ya kuondokewa na
watumishi wake watano ndani ya siku saba, akiwemo Askofu Mstaafu wa Jimbo
Katoliki Bukoba Mhashamu Nestor Timanywa, mapadri watatu na sista.
Taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba
Mhashamu Desderius Rwoma na kuthibitishwa na taarifa kutoka Ofisi ya Katibu
Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) inaeleza kuwa Askofu Nestor
Timanywa amefariki Agosti 28, 2018 saa tano asubuhi katika Hospitali ya Rufaa
Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa.
“Marehemu Askofu Timanywa amekuwa akisumbuliwa na
saratani. Amepatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali na mauti yamemfika
akiwa katika Hospitali ya Bugando Mwanza. Baba Askofu Timanywa ameaga dunia
akiwa na umri wa miaka 81 ya kuzaliwa, 51 ya upadri na 44 ya uaskofu” imeeleza
taarifa hiyo.
Mazishi ya marehemu Askofu Timanywa yanafanyika Agosti
31, 2018 sa tano asubuhi katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama mwenye Huruma,
Jimbo Katoliki Bukoba.
Askofu Timanywa alizaliwa Mei 7, 1937 katika kijiji
cha Kakungiri Parokia yaMugana Bukoba. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri
Desemba 11 1966 na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa. Novemba 26 1973
alitangazwa na Baba Mtakatifu Paulo VI kuwa Askofu wa Jimbo la Bukoba na
akasimikwa Februari 24, 1974. Ameliongoza jimbo la Bukoba kwa zaidi ya miaka 39
hadi alipostaafu Januari 15 2013.
Padri Christian Mhagama
Mnamo Agosti 21 Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga
Mhashamu John Ndimbo alitangaza kifo cha Padri Christian Mhagama, ambacho
kilitokea saa kumi alfajiri katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mazishi ya marehemu Padri Mhagama yamefanyika
Agosti 28, 2018 katika Makaburi ya
Mapadri Kigonsera Jimboni Mbinga, na kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga
Mhashamu John Ndimbo.
Marehemu Padri Mhagama atakumbukwa na wengi hasa
alivyosikika pale alipokuwa mwandaaji na msimamizi wa Kipindi cha ujumbe wa
Biblia kupitia Radio Maria Tanzania.
Akimuelezea Padri Mhagama, Askofu Ndimbo amesema kuwa
watu wamefika kwa wingi kanisani kumuaga kwa sababu ameacha alama kupitia
upendo wake na mafundisho aliyoyatoa kupitia vipawa alivyopewa na Mungu bila uchoyo
unaosababishwa na ubinafsi.
Katika homilia yake Askofu Ndimbo amewaasa waamini
kama wanadamu wanaosafiri hapa duniani, kutoishi maisha ya ubinafsi ambayo
ameyataja kuwa chanzo cha mwanadamu kujitenga na Mungu.
Padri Genesius Kaiza
Mnamo Agosti 23, 2018 Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge
Ngara Mhashamu Severine Niwemugizi alitangaza kifo cha Padri Genesius Kaiza
kilichotokea Alfajiri Agosti 23 saa 10:30 maeneo ya Buseresere akiwa anapelekwa
Hospitali ya Bugando.
Mazishi ya marehemu Padri Kaiza yamefanyika Agosti 25,
2018 yakitanguliwa na
Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la
Kristo Mfalme Rulenge.
Akitoa homilia katika Misa hiyo Askofu Niwemugizi
amesema kuwa imani katika ufufuko ndiyo sababu inayolisukuma Kanisa kuwaombea
marehemu. Amesema kuwa uwepo wa ufufuko ndiyo sababu ya matumaini ya mkristo
mkatoliki.
Padri Ernest Mangwinda
Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi Mhashamu Bruno Ngonyani
amewahimiza wanajimbo hilo kuzidi kumuomba Mungu ili vijana wengi waitikie wito
wa kuwa mapadri na watawa kusudi waendeleze gurudumu la uinjilishaji.
Wito huo ameutoa Agosti 29, 2018 wakati akitoa homilia
kwenye adhimisho la Misa ya Mazishi ya Padri Ernest Mangwinda(65) yaliyofanyika
katika eneo la kuzikia mapadri wa Jimbo hilo lililoko Parokiani Nyangao.
Amesema kuwa kifo cha ghafla cha Padri huyo si tu
kimeacha pengo la wachungaji katika Jimbo hilo, bali pia kinaongeza mzigo mzito
wa kazi ya uchungaji ambayo inawaelemea mapadri wachache waliobakia katika
huduma, mazingira ambayo amewataka waumini wa Lindi kuombea miito ili
wapatikane mapadri wa kutosha.
Askofu Ngonyani amewaambia waombolezaji walioshiriki
adhimisho hilo kuwa, hali ya miito katika Jimbo hilo na hata majimbo jirani ya
Mtwara na Tunduru-Masasi hairidhishi hivyo umuhimu wa kuiombea miito ni mkubwa
siku zetu hizi.
Akizungumzia kifo cha Padri Mangwinda, amesema kuwa ni
cha ghafla, hali ambayo inamdai kila mtu kukesha au kuwa tayari muda wote kwa
ajili ya kukutana na Muumba wake kupitia kifo.
Kwa upande wake Askofu James Almasi wa Kanisa la Anglikana
Masasi, ambaye alihudhuria mazishi hayo aliunga mkono “kilio” cha Askofu
Ngonyani kwa kuwakumbusha wakristo kwenye majimbo ya Lindi, Mtwara na Tunduru
Masasi, wajibu walionao wa kuombea miito kusudi Mwili wa Kristo upate kujengwa.
Padri Ernest Mangwinda alizaliwa huko Namupa katika
Wilaya ya Lindi Vijijini tarehe 10 Machi,1983 katika familia ya watoto nane,
yeye akiwa mtoto wa wanne. Alianza masomo ya msingi hapo Namupa kabla ya
kujiunga na Seminari Ndogo ya Namupa ambako alihitimu masomo ya Sekondari mwaka
1976.
Kwa kuwa bado alikuwa na nia ya kuwa padri, aliendelea
na masomo ya Seminari Kuu Peramiho, Songea hadi Novemba 8, 1983 alipopadrishwa
na Askofu Maurus Libaba(marehemu).
Kutokana na ugonjwa wa ngozi ambao ulimlazimisha
kuhudhuria Kliniki huko Nyangao, na KCMC Moshi, uongozi wa Jimbo ulimpangia
aishi Procure Lindi ambako aliweza kuhudumia Parokia ya Mtakatifu Fransisko
Lindi, mpaka mauti yalipomkuta Agosti 28, huko kwenye Hospitali ya Sokoine
Lindi ambako alipelekwa ili atibiwe.
Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, kifo chake kinaitwa
“Cerebral Vascular Accident”, yaani, ajali ya kupasuka mshipa mkubwa kwenye
ubongo kutokana na shinikizo kubwa la moyo, ambalo halitibiki.
Mazishi hayo yamehudhuriwa pia na Abate wa Ndanda,
Plasido Mtunguja OSB, Abate mstaafu Padri Dionis OSB, na Mapadre wapatao 56
kutoka majimbo la Lindi, Mtwara, Tunduru Masasi na kutoka Jimbo la Anglikana
Masasi, pamoja na idadi kubwa ya Watawa na waamini walei kutoka majimbo hayo.
Sista Suzan
Aidha Agosti 28, 2018 Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya
Bugando alitangaza kifo cha Mkurugenzi wa fedha na mipango wa Bugando Sista
Suzan Bartholomew ambaye alifariki usiku wa kuamkia Agosti 28.
Raha ya Milele uwape Ee Bwana, na Mwanga wa milele uwaangazie, wapumzike
kwa amani, Amina.
Comments
Post a Comment