Fanyeni maamuzi sahihi juu ya imani yenu-Ask. Mdoe
WAAAMINI wa Jimbo Katoliki Mtwara wametakiwa
kufanya maamuzi sahihi katika masuala ya kiimani na kuacha kutangatanga pasipo
kufanya uchambuzi wa kina.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na
Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara Mhashamu Titus Mdoe wakati wa Ibada ya Misa
Takatifu iliyoenda sambamba na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa
la Mtakatifu Paulo Parokia ya Majengo.
Askofu Mdoe amesema hayo kufuatia
uwepo wa waamini wengi wanaohangaika na kuchukua maamuzi katika mambo
yanayohusu imani pasipo kufanya uchambuzi na kubaini ukweli. “Kabla ya kufanya
maamuzi fanyeni uchambuzi na kubaini baya na zuri, kisha baya liache” amesema
Askofu Mdoe.
Aidha amebainisha kuwa wapo watu
wengi katika nyakati hizi wanaotangatanga katika imani na kuwataka kuachana na
kuhangaika bali wawe na misimamo ya kweli katika imani yao hiyo.
Pia katika nafasi hiyo,
amewakumbusha wazazi na walezi kuwafundisha watoto wao kuchagua na kufanya
maamuzi sahihi kwa kuwa huo ni wajibu wao.
Amewataka watoto wote jimboni
humo kuishi katika imani zao na mafundisho wanayopewa kuhusu imani wazingatie
kikamilifu pasipo wasiwasi wowote kwa kuwa imani yao siyo ya kubahatisha.
Comments
Post a Comment