Ask Amani afafanua uvaaji wa shela siku ya ndoa
IMEELEZWA kuwa uchumba siyo
kipindi cha kuvamia haki za ndoa bali ni kipindi cha wachumba kufahamiana,
kuheshimiana na kutunza nidhamu, na hivyo haina maana kwa msichana ambaye
hakutunza usichana wake kuvaa shela siku ya ndoa.
Hayo yamesemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu
Isaac Amani katika homilia yake Dominika ya 5 ya Pasaka hapo Aprili 29, 2018
katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Arusha, ambapo amewasihi
vijana kujitunza vizuri na kuwataka wazazi na walezi kuwasaidia vijana wao
katika makuzi yao.
“Shela ina maana ya ubikira. Wale ambao wametunza ubikira mpka siku ya
ndoa wavae shela. Watakaoruhusu ubikira utoke kabla ya ndoa wasivae shela,
haina maana. Wanaovaa shela ni wale mabikira ndiyo maana ya shela, siyo unavaa
tukuone tu” ameeleza Askofu Amani.
Askofu Amani ameyasema hayo alipokuwa anawahimiza wazazi na walezi juu
ya umuhimu wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu wa Yesu kwa watoto
akisema kuwa shirika hilo linawasaidia watoto kukomaa kiimani na kuwa
wamisionari katika fikra zao.
“Jitunze. Na kama hauna matunzo usivae shela, haina maana. Akikushawishi
mchumba mwambie ninataka nitunze hadhi yangu mbele ya Mungu, dhamiri yangu na
pia kwa wazazi wangu. Mapenzi ya uchumba siyo kuvamia haki za ndoa hapana. Ni
kufahamiana, kuheshimiana na kutunza nidhamu. Na anayekwambia tuharibuharibu
kwanza huyo huyo anakuambia kuharibu kwake siyo jambo la ajabu. Ni ujumbe huo.
Wavulana mjitunze vizuri na wasichana na wazazi msimamie” amesema.
Ataja namna bora ya kusherehekea kipaimara
Aidha Askofu Amani amewaasa wazazi kuwajengea watoto wao mazingira
yatakayowajenga kulingana na mahitaji yao hasa wanaposherehekea komunio ya
kwanza na kipaimara ambapo wazazi wengi wamekuwa na kasumba ya kuwafanyia
watoto wao sherehe katika kumbi na mara nyingine nyakati za usiku.
“Zawadi ya kumpa mtoto wa komunio ya kwanza ni Biblia siyo simu. Mtoto
wa Komunio ya Kwanza apewe Biblia kwa sababu ameshapata misingi ya kuingia
mafundisho ya kipaimara. Hakuna furaha ya mtoto zaidi ya kukaa na watoto
wenzake. Siku ya kipaimara watoto wakae na askofu na kupiga picha na ‘cheers’.
Siku ya mtoto iwe ni ya mtoto na watoto mwenzake wafahamiane, tunawatengenezea
mazingira waendelee kuwa pamoja na kujenga umoja wa kanisa, ni nguvu yetu hiyo”
ameasa.
Pia amesema kuwa mavazi ya kuvaa siku za kipaimara kwa waimarishwa ni
shati jeupe pamoja na suruali na sketi nyeusi na siyo shela kwa kuwa shela
huvaliwa siku ya harusi tena huvaliwa na mwanamke aliye bikira.
Aelezea kaulimbiu yake
Akiielezea kaulimbiu ya utume wake “Mwondoko kuwajibika na kushirikiana
katika Kristo” Askofu Mkuu Amani amewataka waamini jimboni humo kushirikiana na
kujitathmini kiimani wako wapi, katika familia wako wapi, wanakwenda wapi na
nini wafanye ili kufikia malengo yao.
Amewataka wajifunze ushirikiano kama wa mchwa ambao hushirikiana kujenga
kichuguu na kila mchwa hutengeneza tope akitumia mate yake na udongo ikiwa
ndiyo mchango wa kila mmoja katika kichuguu.
“Tembo hathubutu kubomoa kichuguu anakiheshimu, ni kitu imara,
kimejengwa kwa kuwajibika na ushirikiano. Kama mchwa ameweza kufanya hayo kwa
nini sisi wenye zaidi ya mate na udongo tushindwe? Sisi tunaweza zaidi. Leo nazindua
kaulimbiu hii ya awamu ya nne” amebainisha.
Mungu akupe nguvu katika utume wako uendelee hivo hivo Baba.
ReplyDeleteAmina Amina Baba Askofu
ReplyDelete