Waamini msiwamiliki mapadri - Askofu Kassala

Na Marco Kanani, Geita
WAAMINI wameonywa kutowamiliki Mapadri na Mashemasi na kuwafanya kushindwa kutimiza vyema majukumu yao.
Wajibu wao ni kuwaombea kwa Mungu ili utume wao uweze kuwa mwema mbele za Mwenyezi Mungu na kulistawisha Kanisa katika utumishi uliotukuka.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu  Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita wakati akitoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Frateri Didas Kahigi katika Parokia Teule ya Nyehunge jimboni Geita.
Askofu Kassala amesema kuwa, si sawa waamini kuwamiliki Mapadri na Mashemasi kwani ni sawa na kuliangamiza Kanisa kwani kutawafanya watumishi hao wa Mungu kushindwa kutimiza vyema majukumu yao pale watakapokubali kuwa miliki ya baadhi ya waaamini.
Aidha amesisitiza kuwa jambo hilo si jema pia machoni pa Mungu .
Amewahiza waaamini wote kuacha kabisa tabia ya kutamani kuwamiliki Mapadri na Mashemasi huku wakijua wanalo jukumu kubwa la kuwafikia waaamini wote bila kuwabagua ili kuwaelekeza njia njema ya kuona uso wa Kristo.
Pia amewahimiza Mapadri na Mashemasi kujitoa kuwahudumia watu bila kujibakiza, akisema wajue wakipotea wao wamelipoteza Kanisa zima.
Mapadri wajitahidi kuwa wasilikizaji wazuri wa manung’uniko ya watu ya nyakati hizi, yanayohusu siasa, ndoa uchumi na manung’uniko mengine yanawahusu wao kutoka kwa waamini hivyo wayasikilize kwa makini na kuyatolea majibu kwa utulivu.
“Yasikilizeni kwa makini, bila hofu wala woga yatoleeni majibu.  Msiogope kuwakemea hata wanasiasa maana mkiwaacha watararuana na matokeo yake kila kitu kitaenda hovyohovyo. Haipendezi kuacha kuusema ukweli kwa kuogopa kuligusa kundi flani semeni ukweli msiogope, “ amesema.
Mapadri na Mashemasi wajue kuwa waamini wanaowahubiria habari njema ni Dhahabu ya Mungu hivyo dhahabu hiyo waisafishe iwe safi machoni pa Mungu na impendeze .


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI