Suluhu ya maadili kwa mapadri, wanandoa ni malezi kwa vijana

Na Sarah Pelaji, Dar es Salaam
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala ameiasa jamii kuwekeza kwenye malezi kwa vijana ili kutatua changamoto zilizopo katika ndoa, upadri, utawa na katika nyanja zote za jamii.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi, Askofu Kassala amesema kuwa, ulimwengu wa sasa umegubikwa na changamoto mbalimbali kwasababu jamii inazembea malezi kwa watoto na vijana.
“Miito mitakatifu ya Ndoa, Upadri, utawa inaitikiwa na watu ambao wapo tayari kuelekezwa, kutengenezwa na kulelewa ili wamudu maisha waliyoitiwa na Mungu. Upadri pamoja na kuwa ni wito bado unahitaji malezi, uelekezi na kumtengeneza kijana aweze kuwa padri anayehitajika katika jamii.
Analelewa ili awe na tabia zenye utu ndani mwake , upendo, wema, uwajibikaji, uchaji wa Mungu nk.
Seminari hazipokei watu wakamilifu, watu ambao tayari wameshatengenezwa (ready made) hapana ndiyo maana kuna muda wa malezi   ili kijana apate malezi ya kuweza kuuishi upadri wake.
Changamoto ni pale ambapo vijana hawa hawa wahanga wa utandawazi ndiyo hao hao wanapaswa kuwa mapadri, wanandoa na watawa. Kumbe familia ina wajibu wa kuwalea watoto na vijana wao katika malezi sahihi ya jamii.
Tukikosea tu, pale watakapoitikia miito yao, tutapata wanandoa wasio waaminifu na wasiohitajika katika jamii, tutapata mapadri na watawa wasiohitajika katika jamii,” ameeleza Askofu Kassala.
Aidha amesisitiza kuwa, kazi ya jamii ni kufanya malezi maana hata kijana anyefaa anaweza kuharibika kama hajapata malezi sahihi na endelevu.
Pia katika fani mbalimbali za jamii, awe polisi, mwalimu, Daktari nk. anahitajika kijana anayeweza kumudu fani hiyo kwa weledi na nidhamu yake. Jamii ikikosea kuanzia awali kijana akiwa mtoto itateseka kwasababu itakuwa na wahudumu wasio na sifa, wasio na tabia za kibinadamu zenye tunu msingi za uaminifu, wema, uwajibikaji, wenye hofu ya Mungu.
Badala ya kuhudumia watu wanafanya yao yasiyo hitajika na jamii. Hivyo malezi kuanzia ngazi ya familia ni muhimu.
Kila mzazi anaaswa kuzingatia mienendo ya watoto wake, wawaandae kuwa mapadri,watawa, wanandoa na wahudumu wema katika jamii.
“Sikubaliani na kauli za watu kushinikiza kuwa mapadri waoe, kwasababu hata walio na ndoa siyo waaminifu. Kama mwanandoa sio mwaminifu kwa mwenzi wake na wao tuwasaidieje?
Ninachoamini ni kwamba wapo mapadri wengi waaminifu wanaohudumia waamini kwa uaminifu na wanaishi upadri wao ipasavyo. Kama wapo wachache wanaoharibu hawawezi kuhalalisha kwamba sasa useja wa mapadri umeshindikana.
Kadhalika wapo wanandoa wengi wanaoishi ndoa zao kwa uaminifu hivyo hao wachache wanaotoka nje ya ndoa hawawezi kuhalalisha kuwa maisha ya ndoa ni tatizo.
Hivyo tatizo halipo katika kuoa ama kutooa, tatizo lipo katika malezi hivyo suluhu ni malezi katika familia kuanzia utotoni.
Papa Fransisko; Familia siyo gereza dogo
Baba Mtakatifu Fransisko hivi karibuni katika tafakari zake kuhusu maandalizi ya Kongamano la vijana kiulimwengu  anasema, kuna haja ya kujenga mshikamano kati ya wanafamilia na hatimaye majirani katika ujumla wake.
 Kutokana na utamaduni mamboleo, kuna hatari kwamba, familia zinaanza kumeguka na kusambaratika kiasi hata cha kukosa utambulisho na mizizi inayowaunganisha kama jamaa moja!
Kuna haja ya kujenga mazingira yatakayowawezesha wanafamilia kujisikia kweli wako nyumbani na wanathaminiwa na kamwe familia isionekane kuwa kama gereza dogo!
Vijana wapewe fursa ya kujifunza kwa juhudi, bidii na maarifa, lakini pia wapewe malezi yatakayowasaidia kuwajengea heshima, utu wema na uadilifu. Vijana wajengewe uwezo wa kujadiliana na wote katika ukweli na uwazi; wajifunze hekima na busara kutoka kwa wazee wanaoshirikishwa katika  maisha ya kifamilia badala ya kuwatenga kana kwamba, wamepitwa na wakati na hawana jambo ambalo wanaweza kuchangia katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya!
Baba Mtakatifu Francisko anazitaka Familia kuelimisha na kuwafunda vijana wa kizazi kipya, huku wakiongozana nao hatua kwa hatua, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Ujana ni kipindi cha udadisi wenye maswali msingi yanayohitaji majibu muafaka; ingawa wakati mwingine hawana utulivu wa kuweza kusikiliza ushauri wanaopewa! Hii ni sehemu ya maisha ya ujana. Vijana wanapopevuka wanaibua changamoto kubwa katika maisha, lakini hiki ni kipindi muhimu sana kwa wazazi kuwa karibu zaidi na watoto wao!
Ni wakati wa majaribu na hatari za maisha, lakini zaidi ni wakati wa ukuaji wa vijana na familia katika ujumla wake; ni kipindi cha kujenga matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.
 Wazazi na walezi wawe makini, wasiwabane sana watoto wao kiasi hata cha kuchukia maisha.
Ujana si ugonjwa unaopaswa kutafutiwa dawa ya mchunguti anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.
Wazazi na walezi wawasindikize watoto na vijana wao ili waweze kukua na kukomaa, ili hatimaye waweze kushiriki katika kuandaa ustawi na maisha yao kwa siku za usoni.
Katika kipindi kama hiki, vijana wanatamani kuwa marubani wanaoongoza maisha yao.
Ndugu, jamaa na marafiki wa familia wasaidie kukuza na kudumisha tunu bora za maisha ya vijana kwani kuna hatari wakati mwingine, watu wa karibu na familia wakasababisha majanga ya watoto na vijana katika maisha yao.
Wazazi na walezi wawe ni mfano bora wa kuigwa, kwa kuonesha dira, mwongozo na ndoto ambazo vijana wao wanaweza kuzitekeleza katika maisha kwa kutambua pia kwamba, maisha si lele mama kuna changamoto zake; kuna kushuka na kupanda; kuna kusuka na kunyoa! Yote haya yataka moyo kweli kweli! Baba Mtakatifu anazialika Parokia kukuza na kudumisha utume wa vijana, ili kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika maisha yao. Vijana wajengewe uwezo wa kushirikisha karama, vipaji, matumaini hata yale yanayowasambua kutoka katika undani wa maisha yao!
Anawataka vijana kuthamini ujana wao unaojikita katika utu, heshima na nidhamu na wala si ujana wa malumbano na majigambo yasiyo na tija!
Hata leo hii kuna malumbano makali kati ya wazazi na watoto wao! Katika hali kama hii, vijana wengi wanajikuta wanachanganyikiwa kiasi hata cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha.
Kuna baadhi ya wazazi na walezi, wanataka kubaki katika maisha ya ujana kiasi kwamba, hawataki kuzeeka. Hizi ni dalili za watu kukosa maana sahihi ya maisha.
Maisha ni safari inayofanyika hatua kwa hatua kutoka katika utoto, ujana hadi uzee, vinginevyo, jamii inaweza kujikuta ikiwa na wazazi ambao wamedumaa katika maisha.
Vijana wajifunze kuwa na kiasi, kujinyima na kuratibu vionjo vyao. Wakuze kipaji cha ugunduzi kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, umoja na mapendo pamoja na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana.
Vijana watambue umuhimu wa kutumia vyema fursa, nafasi na muda walionao kwani muda ni mali. Umefika wakati kwa familia kujikita katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano; sanjari na kujifunza kuwa watu wenye furaha katika mwelekeo mpya. Wazazi na walezi wanapaswa kujikita katika mchakato wa malezi makini kwa watoto na vijana wao, daima wakiendelea kujiaminisha na kumtegemea Mungu.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU