Kazi ya mama ni kulea miito –Ask. Banzi
Askofu
wa Jimbo Katoliki Tanga Mhashamu Anthony Banzi amewapongeza wanachama wa Chama
cha Mama wa Shauri Jema kwa kusaidia kulea na kukuza miito katika Kanisa.
|
Askofu Banzi amewapongeza akina mama hao
hivi karibuni katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la
Mtakatifu Anthoni wa Padua Chumbageni jimboni humo walipokuwa wakisherekea jubilei ya miaka 25 ya
umoja wao.
Wanashirika hao ambao wameungana kutoka Jimbo
Katoliki Tanga na Morogoro wameaswa kuendeleza malezi kwa vijana kwa manufaa ya Kanisa la Mungu na
nafsi zao.
“Msitishwe na changamoto
mbalimbali zinazojitokeza. Bikira Maria ambaye ni msimamisi wa umoja wenu
awasaidie katika hali zote kwa kufikia maisha ya utakatifu baada ya kufanya
kazi kubwa hapa dunia ya kuwasaidia na kuonesha njia ya imani yenye ukamilifu
mkuu,” amesema Askofu Banzi.
Pia amewataka wanawake wengine
ambao hawajajiunga na umoja huo kujitokeza kwani ni umoja wenye faida kwa manufaa ya Kanisa
kwani kazi ya mama ni kulea.
Amewakumbusha wanaume kujiunga
na wanawake hao kulea miito na pia kujiunga na
mashirika na Vyama vya Kitume ili wapate nafasi ya kujiombea na
kuliombea Kanisa na dunia nzima.
Ikumbukwe kuwa misa hiyo ilitanguliwa
na Mkutano Mkuu wa siku tatu wa kujadili na kupanga mikakati ya kusherekea
jubilei ya mika 25 ya chama cha Mama wa Shauri Jema na wakihitimisha kwa Ibada
ya Misa Takatifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
chama hicho Mama Teodora Mtejeta ameeleza mafanikio wanayojivunia tangu umoja
huo ulipoanzishwa miaka 25 iliyopita na Askofu Thelesphor Mkude wa Jimbo
Katoliki Morogoro ikiwa ni kuendelea kufanya kazi ya kulea miito mbalimbali na
kuongezeka kwa wanachama wapya.
“Sisi kazi yetu kubwa ni
kujitoa katika Kanisa hasa kusaidia kulea miito na hili ndilo lengo la
kuanzishwa kwa chama cha Mama wa Shauri Jema na hivi sasa tumeweza kuunganisha
matawi mawili Tawi la Morogoro na Tawi la Tanga,” amesema Teodora Mtejeta.
Naye Katibu wa Mama wa Shauri
Jema Jimbo Katoliki Morogoro Celina Komba amesema kuwa, umoja wao umelenga
kuongeza wanachama wengi wapya mpaka wafikie 80 ifikapo mwaka 2019 kwani kwa
sasa wapo zaidi ya 60.
Akina mama kutoka majimbo hayo
wanaaswa kujiunga na chama hicho ili kulea miito katika Kanisa kwani mama ni
mlezi katika jamii.
Roho Mtakatifu awaongoze mzidi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuenea sehemu nyingi katika Tanzania.
ReplyDelete