Kila muumini awe mmisionari-Padri asisitiza
|
WANAUTUME wa Fatima hapa nchini, wameelezwa kuwa
kupitia ujumbe wa Fatima uliotolewa na Bikira Maria kule Ureno alipowatokea Watoto
wa Tatu, Russia, Fransisko na Yasinta wanaalikwa kuwa wamisionari wa kweli na
hasa kuwaombea wale wote wasiomwamini Kristo, ili wapate kumwamini na kufuata
matendo yake.
Wito huo kwa Wanautum hao wa Fatima umetolewa na Padri
Evans Msechu, wakati akiadhimisha sadaka ya Misa Takatifu kwenye adhimisho la
siku ya Bikira Maria Mama yetu wa Fatima iliyofanyika katika Parokia ya
Msimbazi Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam.
Padri Msechu ambaye ni katibu wa Ndugu wadogo wa
Fransiskani amesema kuwa, Mama Bikira Maria ni mmisionari wa kwanza, na kwa
kuwa Wanautume wa Fatima wanamwakilisha yeye hawana budi kuwa wamisionari
katika maisha yao yote na mahali popote pale wanapokuwa.
Aidha ameongeza kuwa wanautume wa Fatima wanapaswa
kutambua kuwa wao ni mabalozi, na kazi kubwa ya Balozi ni kuwakilisha jamii
kubwa iliyoyuma yake, na sasa watambue kuwa wanayo kazi kubwa ya kuhakikisha
wanaombea amani ndani ya familia, jumuiya parokia, taifa na hata ulimwengu
mzima, na si kujiombea wao wenyewe tu.
Padri Msechu ameeleza kuwa, kwa kuwa wanautume wa Fatima
ni mabalozi wa Mama Bikira Maria, wahakikishe watu wanamuona Bikira Maria
pamoja na Yesu Kristo ndani ya mioyo yao kupitia kazi yao wanayofanya, matendo
yao, na hata kuongea kwao.
“Wewe ndiwe balozi wa Mama Maria, maana yake pale unapofanya kazi
unamwakilisha Mama Maria, sehemu ambayo Maria alikuwa aende akafanye kazi wewe
unafanya badala yake, kwa hiyo ongea yako iwe ni ya Kibira Maria, kazi yako
unayofanya mtu atambue na amuone Kristo na Bikira maria ndani yako,” alisema Padri
Msechu.
Padri Msechu amehitimisha mahubiri yake kwa kuwataka
wanautume hao wa Fatima kuendelea kumuomba Mama Bikira Maria aendelee
kuwasindikiza na kuwaombea,ili wahusianishe maisha yao na kile walichonacho na
kufanya mageuzi ya ndani ya mioyo yao na si mageuzi ya nje, na pia waendelee
kujikita katika kusali kwani dunia ya leo isipokuwa na amani watambue kuwa wao
utume wa Fatima ndio shida kwamaana wameshindwa kusali zaidi.
Adhimisho la Misa takatifu siku ya Bikira Maria Mama yetu
wa Fatima, lilitanguliwa na maandamano ya Rozari Takatifu, maungamo,
mafundisho, pamoja na kuabudu na Ekaristi Takatifu, ambapo Padri Msechu alikuwa
akishirikiana na Padre Gidion Peter Mboya Paroko Msaidizi wa Parokia ya
Msimbazi ya Bikira Maria Mama wa Fatima.
Comments
Post a Comment