Ask. Lebulu: Tuwapende hata wale wanaotupiga vita

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Mhashamu Josaphat Lebulu amesema kuwa huruma ya Mungu inatoa fursa kwa wanadamu kudumu katika upendo, kwa kuwapenda hata wale wanaowapiga vita, kama Mungu alivyo tayari kuwasamehe wema na wabaya.
Ameeleza hayo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kufunga Mwaka Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu jimboni Arusha, lililofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Thereza, na kuhudhuriwa na mamia ya waamini wa jimbo hilo.
Askofu Lebulu amesema kuwa baada ya kufungwa kwa yubilei hiyo, waamini wanaalikwa kutoka na kuionesha huruma ya Mungu kwa watu wote hasa wanaoihitaji zaidi. Ametoa rai kwa waamini hao kuitambua huruma ya Mungu, inayotenda kazi kati ya watu na ndani ya watu.
“Leo tunafunga yubilei ya huruma na siyo kufunga huruma ya Mungu. Tunafunga yubilei na sasa tuendelee mbele tukiwa kama watu tuliofaidi huruma ya Mungu. Tuendelee na hamasa tuliyoionja katika fursa mbalimbali kama makongamano na hija” ameeleza Askofu Lebulu.
Aidha Askofu Lebulu ametoa rai kwa waamini kuwa tayari kusamehe wengine, na kupokea msamaha kutoka kwa wenzao, ili waweze kuushinda ubaya kwa wema.

Pia amewatoa mashaka waamini ambao wanajihoji iwapo watadumu katika mema waliyoyachuma ndani ya mwaka wa huruma ya Mungu, na kuwaambia kuwa hawana budi kujipa moyo na kusonga mbele kwa kuwa Kristo wanayemtumaini ameushinda ulimwengu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU