JUBILEI YA WAKLERI YAANZA KUTIMUA VUMBI MJINI VATICAN
Wakleri na majandokasisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuanzia tarehe 1- 3 Juni 2016 wanaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuungana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi na wito wa Daraja Takatifu, mwendelezo wa utume wa Kristo Yesu katika: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kilele cha Jubilei ya Wakleri na Majandokasisi ni hapo tarehe 3 Juni 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Wakleri Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 25 machi 1995. Katika barua hii, Mtakatifu Yohane Paulo II kwa namna ya pekee, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa utakatifu wa maisha ya wakleri kama chachu muhimu sana kwenye mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha. Ulimwengu mamboleo unahitaji wainjilishaji wapya, wenye ari na moyo mkuu, wanaofumbata zawadi ya wito na maisha ya kipadre kama hija inayowaelekeza kwenye utak...