Papa Francisko atangaza nia ya kutembelea Iraq 2020
shirika
la Misaada kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki, ROACO Juni
10 mwaka 2019 limeanza mkutano wake wa tisini na mbili kwa kukutana na
Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatikani.
Tangu mwaka 1968, ROACO kimekuwa ni chombo cha
upendo na mshikamano kinachoratibiwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa
ya Mashariki. Ni huduma inayotekelezwa kwa namna ya pekee kupitia pia Mabalozi
wa Vatikani katika nchi hizi bila
kusahau mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Wafranciskani waliopewa dhamana
ya kulinda maeneo matakatifu.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amegusia
yale yaliyojiri tangu walipokutana mara ya mwisho: umuhimu wa kuendeleza Injili
ya huduma ya upendo kwa maskini na waathirika wa vita na mipasuko ya kijamii;
changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita
pamoja na mchakato wa Kanisa kuendelea kuwekeza katika Injili ya matumaini
miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baba Mtakatifu ametumia fursa hii
kuwapongeza wajumbe wa ROACO kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya
kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini ya leo na kesho iliyo bora kwa
Makanisa ya Mashariki ya Kati!
Tangu walipoachana mara ya mwisho, Mwaka
Jana, 2018, kumekuwepo na matukio kadhaa katika maisha na utume wa Kanisa. Baba
Mtakatifu anasema, amepata fursa ya kujionea mwenyewe Injili ya huduma wakati
wa hija zake za kitume huko Bulgaria, Macedonia ya Kaskazini pamoja na Romania.
Kwa namna ya pekee kabisa, anakumbuka mkutano wa Sala ya Kiekumene kwa ajili ya
Kuombea Amani huko Mashariki ya Kati, ulioadhimishwa mjini Bari, tarehe 7 Julai
2018. Ilikuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukutana, kusali na kutafakari pamoja
na ndugu zake wakuu wa Makanisa kutoka Mashariki. Baba Mtakatifu anaendelea
kusema kwamba, mkutano mkuu wa ROACO ni fursa ya kusikiliza na hatimaye kujibu
kilio cha watu waliopokonywa Injili ya matumaini katika maisha yao, kama ilivyo
huko nchini Siria, ambako hali bado ni tete sana.
Kuna watu wanaoteseka kutokana na uhaba wa
chakula na lishe bora; ukosefu wa huduma za afya na elimu pamoja na umati
mkubwa wa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.
Hawa ni watu ambao wamejeruhiwa sana nyoyoni mwao, lakini wanayo nafasi ya
pekee moyoni mwa Mwenyezi Mungu! Wale ambao wamejeruhiwa wanaweza kukimbilia na
kupata hifadhi; huruma, upendo na nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye kwa
hakika ni Baba anayewapenda na kuwalinda watoto wake! Baba Mtakatifu anaonya
kwamba, iko siku, hasira ya Mungu itawawakia viongozi wanaozungumzia amani,
lakini kwa upande mwingine ni wa kwanza kuuza silaha ambazo zinaendelea
kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu. Huu ni unafiki na
dhambi kubwa machoni pa Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda
kuyaelekeza mawazo yake kwa familia ya Mungu nchini Iraq, ambako anatarajia kwenda kufanya hija ya
kitume mwaka 2020,Mwenyezi Mungu akipenda. Baba Mtakatifu anatumaini kwamba,
mchakato wa kutafuta na kudumisha amani, ustawi na mafao ya wengi, utasaidia
kuvunjilia mbali chuki na uhasama unaokita mizizi yake katika migogoro ya
kidini katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini kimsingi ni mgogoro unaojikita
katika uchu wa madaraka. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, awamu ya pili
ya ukarabati wa Kaburi Takatifu utaweza pia kuwashirikisha kwa namna ya pekee
Wakristo pamoja na viongozi mahalia, ili hatimaye, haki, amani na maridhiano
yaweze kutawala kati ya watu, kama alama ya baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi
Mungu!
Baba Mtakatifu anasema, kuna kilio cha
wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta matumaini, lakini hakuna nchi ambayo iko
tayari kuwapokea. Bandari zimefungwa kwa wakimbizi na wahamiaji, lakini malango
yake yamefunguliwa kwa meli zinazobeba silaha ya maangamizi na zenye gharama
kubwa zinazoendelea kusababisha maafa makubwa! Huu ni unafiki mkubwa. Hiki ni
kilio cha Abeli kinalomfikia Mwenyezi Mungu. Hawa ni watu wanaotafuta neema,
baraka na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu hawa ni Uso wa Kanisa,
unaopaswa kupyaishwa, kwa kutangaziwa na kushuhudiwa Injili ya matumaini, kama
walivyokazia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa
kunako mwaka 2018.
Vijana wanapokutana na mashuhuda aminifu na
wa kweli, hawana sababu ya kuogopa na kwamba, wako tayari kujisadaka bila ya
kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake! ROACO iendelee kuwa mstari
wa mbele katika mchakato wa malezi na makuzi ya vijana kiutu na kimaadili na
kamwe wasikubali kutekwa na ukoloni wa kiitikadi; wazamishe mizizi ya maisha
yao katika mila, tamaduni na mapokeo ya nchi zao, daima wakiwa mstari wa mbele
ili kuhakikisha kwamba, amani, ustawi na maendeleo yanapatikana kwa ajili ya
wote na wala hakuna mtu awaye yote anayeachwa nyuma!
Baba Mtakatifu anasema, kwa mara ya kwanza
katika historia, vijana kutoka Ethiopia na Eritrea watashuhudia kuzimika kwa
mlio wa silaha, tayari kuanza mchakato unaofumbatwa katika ujenzi wa udugu wa
kibinadamu; kwa kuheshimiana na kuthamianiana kama ndugu wamoja kama
inavyosisitizwa kwenye Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa mkwaju kati yake
na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini
Misri ni mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na
kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha
misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa ROACO
kumsaidia kusambaza ujumbe wa Agano hili, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na
mafao ya wengi. Watu wote wajisikie kwamba wanahusika kikamilifu katika
kutekeleza yale yaliyotajwa kwenye hati hii. Dhamana hii ipewe kipaumbele cha
pekee anasema Baba Mtakatifu na wadau katika: taasisi za malezi na majiundo ya
vijana wa kizazi kipya, hasa huko Lebanon na Mashariki ya Kati. Lengo liwe ni
kuwawezesha vijana kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na maridhiano
kwa watu wote.
Comments
Post a Comment