Askofu Ruzoka awafunda waseminari waliohitimu Falsafa Kipalapala
Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Mashamu Paul Ruzoka amwewaasa Mafrateri wa
seminari Kuu Ya Mtakatifu Paulo Mtume Kipalapala kuwa waaminifu kwa Neno la
Kristo na kumfuata Kristo kwa kuishi maisha ya ufukara na kukaa mbali na mali
za dunia.
Rai hiyo ameitoa hivi karibuni katika
Kanisa la seminari hiyo alipokuwa akitoa mahubiri yake yaliyolenga kumshukuru
Mungu kwa neema nyingi alizowajalia mafrateri wa mwaka wa nne waliohitimu
malezi yao seminarini hapo.
Akizungumza wakati wa Misa Takatifu Askofu
Mkuu Ruzoka amewahimiza mafrateri hao wanaoenda kufanya utume wao katika sehemu
mbalimbali za majimbo ya Tanzania kuishi yale walioyapata wakati wa malezi yao
. “ Nendeni mkatoe harufu nzuri ili kwa wale mtakaowahudumia wamuone Kristo
kupitia nyie”, Askofu Ruzoka amesema.
Aidha katika mahubiri yake Askofu Ruzoka
amewaomba mafrateri wahitimu kujua sasa wameongezeka kimo na ufahamu hivyo
hawanabudi kutumia elimu na maarifa waliyoyapata kwa faida ya Kanisa na
wanapaswa kuhakikisha kundi la waamini linaongezeka.
Pia ameelezea wajibu wa kwanza wa wahitimu
hao ni kuhakikisha wanahamasisha miito ya Upadri na utawa popote watakapokuwa
kwani uhai wa Kanisa unategemea sana idadi wa vijana walioko katika seminari
zetu majimboni.
Aidha amewataka mafrateri hao wahitimu
kutoa huduma yao kwa bidii, upendo na huruma kwa wote wataokutana nao katika
mwaka wao huo wa uchungaji na baadae kama mapadri.
Amewataka kutumia ukomavu na busara kwani
wanakokwenda hakuna uzio kama huu wa seminari bali wawe wakomavu na watu
wenyekupima mambo.
Sambamba na kumshukuru Mungu pia katika
Adhimisho la Misa Takatifu, Gambera wa Seminari hiyo Kuu Mh. Hermani Kachema
alithibitishwa kuwa Gambera wa Seminari ya Kipalapala na kuendelea na utume
wake ambao alishauanza tayari.
Mara baada ya Misa Takatifu ilifuata
michezo na burudani mbalimbali ukumbini iliyohudhuriwa na wageni toka parokia
mbalimbali za jimbo kuu Tabora.
Comments
Post a Comment