Huwezi kutenganisha utume wa walei na maendeleo ya Kanisa- Kard.Pengo asema
IMEELEZWA
kuwa waamini walei nchini wamekuwa chachu ya maendeleo ya Kanisa kwa ushiriki
wao kikamilifu katika mipango na utekelezaji wake katika hatua mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya utume wa
walei Tanzania, yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Msimbazi Center
jijini Dar es salaam na kufikia kilele chake Juni 16, 2019.
Kardinali Pengo ameeleza kuwa walei
hawapaswi kujiona kuwa ni watu wa kuambiwa tu kana kwamba hawana mchango
wowote, bali wanapaswa kuona kuwa wao ni sehemu muhimu ya maendeleo ya Kanisa.
“Kabla ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani
waamini walei walisubiri watekelezewe kila kitu kana kwamba hawana chochote cha
kutoa. Baada ya mtaguso huo Kanisa limetambua nafasi ya walei na hivyo ni
lazima wajue kuwa wana sehemu muhimu ya kufanya, siyo tu kulipa zaka na
kusikiliza maelekezo” ameeleza Kardinali Pengo.
Aidha Kardinali Pengo ametumia fursa hiyo
kuwakaribisha waamini kutoka majimbo yote nchini kushiriki kikamilifu katika
maadhimisho hayo kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa jubilei hiyo.
Pia ametoa mwito kwa waamini kushiriki
matukio mbalimbali yanayotangulia kilele cha jubilei hiyo ikiwa ni pamoja na
semina mbalimbali zitakazotolewa na maaskofu na watu walioandaliwa, ikiwa ni
njia moja wapo ya kuadhimisha miaka 50 ya utume wa walei.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Idara
yaUtume wa Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raphael
Madinda ameeleza kuwa uwepo wa walei katika Kanisa umekuwa chachu ya kuongezeka
kwa miito mitakatifu ambayo inachipuka kupitia familia.
Amesema kuwa kupitia familia ambao ndio
walei ndiko Kanisa linapata miito mbalimbali kama vile upadri na utawa, huku
akitoa wito kwa waamini walei kuendelea kuziimarisha familia zao kwani mchango
wake katika ustawi wa Kanisa ni mkubwa.
Comments
Post a Comment