Wanaume Katoliki DSM waanzisha Bima ya Afya, Maisha

Askofu Mkuu Mwandamizi  wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Jude Thadeus Ruwaichi akimkabidhi Mwenyekiti wa UWAKA Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Ndugu Amedeus Mosha kadi za Bima ya Afya  mara baada ya kuzindua Mradi huo Dar es  Salaam katika sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa Wanaume Wakatoliki iliyofanyika katika  kituo cha hija Pugu (Picha na Philipo Josephat)




Na. Philipo Josephat-Dar es Salaam
Umoja wa Wanaume wakatoliki wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam umeanzisha Bima ya Afya na Bima ya Maisha.
Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi amezindua kadi za Bima hizo hivi karibuni baada ya kuhitimisha Ibada ya Misa Takatifu siku ya wanaume katoliki (UWAKA) katika Sherehe ya Msimamizi wao Mtakatifu Yoseph iliyofanyika kwenye kituo cha hija Pugu  jiji Dar es Salaam.
 Askofu Ruwaichi amewapongeza wanaume Katoliki Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam kwa ubunifu mkubwa wa kuanzisha Kampuni ya Bima ya Afya na ya maisha  itakayowasaidia waamini na watu katika hali tofauti za maisha yao.
Aidha amewataka waendelee na ubunifu mbalimbali na kubuni Bima ya Elimu itakayo wasaidia watoto wengi wanaokosa haki ya elimu.
“Bima ya Elimu ni ya muhimu sana kwani itasaidia watoto hasa kutoka kwenye kaya masikini kupata elimu kwa urahisi na uhakika.  Endapo UWAKA  mtafanikisha hili linaweza kustaajabisha watu na taifa,” amesema.
Kwa upande mwingine, Askofu Ruwaichi ameonesha kutoridhishwa na ushiriki wa wanaume katika jumuiya Ndgondogo za Kikristo.
 Amesema tangu afike katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam na kuzitembelea jumuiya ndogo ndogo amekutana na changamoto ya wanaume kutohudhuria kwenye Jumuiya ndogondogo  na kusema kuna haja ya kuchukua hatua ili kukomesha tatizo hili kwa wanaume.
Amewataka wanaume wakatoliki (UWAKA) kubadilika na kuwa watu wa kuhudhuria Jumuiya ndogondogo za Kikristo ili kuimarisha Kanisa.
Amesema kuna haja ya kuchukua mawasiliano ya simu ili pindi inapofika ijumaa wakumbushwe  kuhudhuria ibada za jumuiya.
Aidha katika homilia yake kwa wanaume wote wakatoliki waliohudhuria ibada hiyo na kusindikizwa na akina mama na watoto Askofu Ruwaichi amesema ukimwacha Bikira Maria Mtakatifu Yosefu ndiye Mtakatifu maarufu zaidi kuliko wote na ili mtu aweze kuyajua haya hanabudi kuyapapasa Maandiko Matakatifu.
Amesema kuwa, Mtakatifu Yoseph kama baba wa Familia Takatifu alikuwa mtu wa haki hivyo akina baba wote wanatakiwa kuwa watu wa haki kama alivyo somo na msimamizi wao.
“Haki ni kumpa kila mmoja mastahili yake, Mt.Yoseph alikuwa mtu wa haki, je wewe baba, mtawa, ni mtu wa haki? Mungu anayomastahili yake kwetu, ametuumba, anatutawala, ana haki ya kutumikiwa na kuheshimiwa ni katika namna hiyo tunampa Mungu mastahili yake,” amesema.
Askofu Ruwaichi amewataka wanaume wajue kuwa wao ni muhimili katika Taifa hivyo wanapaswa, kulilinda na kulitegemeza Kanisa kwa vipaumbele vilivyopo sanjari na mumwombea Baba Mtakatifu aliongoze vema Kanisa na kuliombea Jimbo.
Mtakatifu Yosefu ni msimamizi wa wanaume wakatoliki wote, hivyo kila mwaka wanaume wa Jimbo Kuu Katoliki  Dar es Salaam huadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya somo wao katika viwanja vya hija Pugu na kwa mwaka huu ibada imeongozwa na Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki La Dar Es Salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi na Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo hilo pamoja na mapadri na watawa na wa kike.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU