Benki ya Mkombozi yafungua tawi Iringa
Benki ya Biashara ya Mkombozi
imefungua tawi mkoani Iringa ikiwa ni utekelezaji wa mipango ya Benki hiyo
kupanua huduma zake ili kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.
Akifungua tawi hilo, Askofu wa wa
Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amewataka waamini wa
jimbo hilo, wananchi na watu wenye mapenzi mema kuitumia Benki ya biashara ya
Mkombozi ambayo imeanza kutoa huduma zake mkoani humo.
Benki hiyo inatoa huduma
mbalimbali za kibenki ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa vikundi, mtu binafsi,
taasisi na mashirika mbalimbali.
Tawi hilo la Iringa ni kati ya
matawi 10 ya Benki hiyo lengo ikiwa ni kuenea nchi nzima.
Awali, Askofu Ngalalekumtwa
ameyabariki majengo ya Benki hiyo yaliyopo kwenye Chuo Kikuu cha Kanisa
Katoliki cha Ruaha (RUCU) na amesisitiza umuhimu wa kuweka akiba kwenye benki.
“Tulitamani sana kuidhisha lile
ambalo tumeidhinisha leo hii, benki ambayo tumeishughulikia sasa imefunguliwa
hapa kwetu, ni nafasi ya benki hii kutulea huduma kwa karibu na sisi wananchi
tujijengee utamaduni wa kuweka akiba kwa
matumizi mbalimbali,” amesema Askofu Ngalalekumtwa.
Aidha amewataka watendaji wa
benki hiyo kuwa wabunifu na kutoa huduma kwa weledi kulingana na taratibu za
benki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo
Bw. George Shumbusho amesema kwamba Benki hiyo mwaka huu Agasti 27 itakuwa
ikiadhimisha miaka 10 tangu ianzishwe na Kanisa Katoliki Tanzania kutoa huduma
kwenye maeneo mbalimbali nchini.
“Ndoto yetu ya kutoa huduma
nyanda za juu kusini imekamilika ni wazi pia uchumi wa Iringa na watu wote
wa maeneo haya utazidi kuimarika baada
ya kufungua benki hii hapa kwenu,” amesema Bw. Shumbusho .
Amesema kwamba kutokana na benki
hiyo kuadhimisha miaka hiyo 10 ni wazi
kwamba benki hiyo ni komavu katika kutoa huduma kwa kiwango kinachoridhisha
hivyo wamejipanga vizuri kutoa huduma bora zaidi.
Ametoa ombi kwa wakazi wa maeneo
hayo kuitumia benki hiyo ambayo ina weledi mkubwa kwenye huduma za kibenki.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Kikatoliki Ruaha RUCU, Dr Pd. Pius Mgeni amesema kwamba hakuna Benki ambayo ina
jina kubwa kama Benki ya Mkombozi kwani imekuja kuwakomboa wananchi wa mkoa huo
kiuchumi.
Pd. Mgeni amesema kwamba wapo
tayari kushirikiana na benki hiyo katika kuimarisha uchumi wa Iringa.
Akizungumza na Gazeti hili,
Meneja Masoko wa benki hiyo Bw. Andrew Chimanzi amesema kuwa, wamefungua
milango ya benki hiyo kwa wateja wao ambao walikuwa wakisubiri kwa muda mrefu
huduma za benki hiyo.
“Hii ni benki ya biashara ina
kibali cha kufanya huduma zote za kibenki ikiwemo, kufungua akaunti, mikopo kwa
wafanyakazi, mikopo mikubwa na midogo na kwa wajasiriamali wadogo pia.
Wito wangu kwa wana Iringa waje
tuwahudumie, wafanyakazi wetu wana weledi wa kutoa huduma za kibenki hivyo
tunawakaribisha,” amesema Bw. Cimanzi.
Comments
Post a Comment