Ukeketaji, umasikini, ugomvi wa wazazi chanzo cha watoto kuzikimbia familia
Umasikini, ukeketaji na kuvunjika kwa ndoa katika
familia kumetajwa kuwa ndio chanzo cha watoto wengi kukimbia familia zao
na kujikuta wanakuwa wa mitaani.
Pia hali hiyo imetajwa kuchangia watoto
wengine kuzikimbia familia zao na kulelewa katika vituo vinavyowasaidia
watoto wenye mahitaji maalum.
Hayo yamesemwa na wasichana 15 waliohitimu mafunzo ya fani mbalimbali ya
stadi za maisha wa kituo cha Jipe Moyo kilichopo katika Parokia ya Mwisenge
Jimboni Musoma ambao walikimbia ndoa za utotoni, Ukeketaji, waliobakwa na
kufanyiwa vitendo vya ukatili na hatimaye kukimbia familia zao na kulelewa na
kituo hicho kwa zaidi ya maiaka miwili.
Msimamizi wa Kituo hicho Sr Maria Annunciata
Chacha amesema kwa sasa kituo kina zaidi
ya watoto 130 wanaohudumiwa na wanakabiliwa na upungufu wa chakula.
Hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia chakula walau hata mlo mmoja kama ni mchana au usiku maana
wanaelemewa na watoto baada ya idadi kuongezeka.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma Fidelica
Myovella amesema ni kweli kituo kinajitahidi sana kuwalinda watoto kwani wengi
waliopo katika kituo hicho wanatoka katika mikoa mbalimbali na wilaya zote za
Mkoa wa Mara.
Hivyo wao kama serikali
watawasaidia hata kuwapatia mikopo ili waweze kuendelea na ujasiriamali pamoja
kwa kuanzisha kikundi chao sambamba na kutoa elimu kwa jamii.
Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk Vicent Naano
amesema wataangalia namna ya kusaidia kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuwapatia
mlo mmoja wa chakula,kuwasaidia cherehani kwa ajili ya ushonaji, na mahitaji
mengine kwani alikuwa hajui kama wana
changamoto kubwa kiasi hicho.
Amewaomba wasimamizi wa kituo
hicho kuanzisha fani mbalimbali kama ufundi wa ujenzi wa nyumba, umeme na
kuchomelea vyumba (welding), ili kupanua wigo kutokana na watoto wanaokuja
kituoni hapo kuwa na vipaji tofautitofauti,huku suala la upungufu wa chakula
kituoni hapo akiahidi kwenda kulifanyia kazi.
Comments
Post a Comment