Viongozi wa dini watangaza vita dhidi ya ukatili wa kijinsia


Na Pascal Mwanache, Dar

VUGUVUGU la kiimani kwa ajili ya kutetea usawa wa kijinsia na kupinga ukatili wa kijinsia nchini limezinduliwa jijini Dar es salaama hivi karibuni, ikiwa ni nguvu ya pamoja ya viongozi wa dini na wadau mbalimbali katika kuibadilisha jamii iondokane na mila zinazochochea ukatili.
Vuguvugu hilo linaloitwa ‘Side by side’ yaani ‘bega kwa bega’ limezinduliwa Novemba 30, 2017 katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es salaam, ambapo wadau mbalimbali na viongozi wa dini wameeleza kuwa uwepo wa vuguvugu hilo utasaidia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Rev. Moses Matonya amesema kuwa lengo la vuguvugu hilo ni kuweka nguvu za pamoja kama viongozi wa dini kwa kushirikiana na wadau wengine ili kupinga ukatili wa kijinsia.
Amesema kuwa wanaunga mkono jitihada za serikali na wadau katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuihimiza jamii na kuielimisha ili ibadilike na kuachana na mila potofu zinazochochea ukatili.
“Tunalenga kuibadilisha jamii iache vitendo vya ukatili kwa watoto, wanawake na wanaume, tukikemea lugha za matusi na udhalilishaji wa utu wa binadamu. Ukatili unaweza kutokomezwa ikiwa jamii yenyewe itaamua na kuyapa kipaumbele masuala yanayohusu usawa wa kijinsia. Nasi kama viongozi wa dini tunawiwa kutafsiri neno la Mungu kwa mtazamo wa kijinsia na kuachana na mila kandamizi. Pia tunalenga kuihamasisha jamii kusema hadharani juu ya vitendo vya udhalilishaji” ameeleza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe amewapongeza wana vuguvugu la ‘bega kwa bega’ akisema kuwa ukatili wa kijinsia ni changamoto kubwa hapa nchini kama ilivyo katika nchi nyingine, na kusema kuwa vuguvugu hilo linaenda sambamba na maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Aidha amesema kuwa jitihada hizo zitasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ambapo idadi ya vifo hivyo inaongezeka ambapo mwaka 2010 ilikua asilimia 23 na 2015 ilifikia asilimia 27.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU