KANISA TABORA LAANZISHA KILIMO CHA KOROSHO, MAEMBE
JIMBO
Kuu Katoliki Tabora hivi karibuni limezindua kilimo cha korosho na miembe ya
muda mfupi katika eneo lake la hija ili kutoa mfano wa kilimo cha
kibiashara.
Akiongea na Gazeti hili kwa niaba ya Askofu Mkuu Paul
Ruzoka, mhasibu wa jimbo hilo Padri Nicolaus Bulabuza amesema kuwa Jimbo Kuu
Tabora limeamua kuanzisha kilimo cha korosho na miembe ya muda mfupi ili kutoa
elimu kwa wanatabora kubadili mawazo na kuona bado Tabora inaweza kuingia
katika kilimo hiki kipya.
Aidha Padri Bulabuza amesema kuwa wao kama Kanisa hawana
budi kuona ni kwa namna gani wanaweza kuunga mkono kauli mbiu ya serikali ya
awamu ya Tano yaani Tanzania ya viwanda. “Kila mwana Tabora hana budi
kuona yeye anaingiaje katika mnyororo wa Tanzania ya viwanda,” ameongeza.
Akifafanua zaidi Padri Bulabuza amesema mazao ya korosho na
miembe hayana budi kupewa kipaumbele kwani yana faida nyingi baadhi yake ikiwa
ni kutumika kama chakula, na pia ni biashara.
Pia amesema kuwa wana Tabora hawana budi kupokea mazao hayo
kwa mikono miwili ili kujiongezea chakula na kipato cha kaya, wilaya, mkoa na
hatimae Taifa. Hii imetokana na wana Tabora wengi kujikita katika kilimo
cha tumbaku kwa muda mrefu kitu ambacho kimesababisha uharibifu wa mazingira na
afya kwa wakulima.
Padri Bulabuza amesema kilimo cha korosho na miembe ni
rafiki wa mazingira tofauti na zao la tumbaku ambalo kwa miaka mingi limeicha
Tabora katika hali mbaya kimazingira.
Kilimo hicho kilichozinduliwa chini ya Afisa Ugani wa kata
ya Ifucha katika Manispaa ya Tabora, ni mategemeo kuwa mashamba hayo yatakuwa
darasa kwa wanakijiji wa kijiji cha Ifucha na vitongoji vyake.
Jimbo Kuu Tabora tayari limepanda zao la korosho kwa ukubwa
wa Ekari 4, na Ekari mbili za miembe ya muda mfupi.
Comments
Post a Comment