ELIMU IWE CHOMBO CHA KUMKOMBOA MWANADAMU


ASKOFU wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amesema kuwa, elimu ni chombo cha ukombozi kwa mwanadamu na iwapo ataikosa anapungukiwa uelewa na uwezo wa kuyatawala mazingira anamwoishi.

Askofu Ngalalekumtwa ameyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Katibu wa Elimu Jimboni humo Padri Dkt. Pius Mgeni kwenye kikao cha mameneja na wakuu wa shule zinazomilikiwa na Jimbo hilo uliofanyika katika ukumbi wa kichangani senta ya vijana.

Mhashamu Ngalalekumtwa amesema kwamba binadamu asiye na elimu hawezi kutoa mchango wake kuindeleza familia ya mwanadamu (jumuiya).

“Kanisa linatambua wajibu wake wa kumfanya mwanadamu afurahie ile zawadi na heshima aliyopewa kama mwana wa Mungu, ndiyo sababu wamisionari wetu toka kuingia kwao nchini mwetu walijenga na kuendesha shle katika ngazi mbalimbali, kuanzia elemu ya  awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi na ualimu, hadi sasa tumefikia elimu ya juu.

Jimboni kwetu utume kwa njia ya elimu unabebwa na parokia, watawa na hata vikundi binafsi kazi ambayo siyo rahisi kwani ni sadaka nzito kuwa na rasilimali watu, miundombinu na fedha za uendeshaji, samani, na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Uchumi wa leo umekuwa mgumu kwa wote, yaani wazazi na wamiliki wa shule..pamoja na nia njema tunafikia wakati ambapo tunaelekea kukwama.

Elimu inadai mpangilio katika sekta zote, ndiyo sababu serikali inaandaa sera ya kuratibu elimu nchini.  Nalo Kanisa kama mdau linaandaa sera ya elimu ili misingi ya Injili izingatiwe” amesema na kuongeza kuwa “ katika kutekeleza hilo Kanisa Katoliki nchini mwetu (T.E.C.) linashirikiana na Makanisa mengine (C.C.T.) katika ile Tume ya Huduma za Jamii za Kanisa (Christian Social Services Commision CSSC)”.

Mhashamu Ngalalekumtwa amesema kwamba katika ngazi ya Jimbo wanaagizwa kuwa na sera inayoratibu utekelezaji wa maagizo, maamuzi na makusudio au malengo ya elimu kutoka ngazi za juu.

Katika kikao hicho mameneja na wakuu hao wamepitia sura nane (8) za sera ya elimu Jimbo la Iringa, pamoja na mambo mengine, Pd. Mgeni amewataka wamiliki hao kuendesha shule zao inayoendana na kanuni, taratibu na sheria za  Kanisa Katoliki.

Katika kikao hicho washiriki hao waliunda kamati ya Elimu Jimbo, mwenyekiti wake akiwa ni Pd. Pius Mgeni, katibu ni Francis Mwilafi na Mhazina ni Sr. Matrida Chuhila wa Shirika la Wateresina wa Mtoto Yesu (CST).

 Na Getrude Madembwe, Iringa.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU