Kumbukumbu ya miaka 15 tangu Mt. Papa Yohane Paulo II afariki dunia


KAnisa Katoliki duniani Aprili 2 mwaka huu linakumbuka miaka 35 tangu Papa Yohane Paulo II (sasa Mtakatifu) afariki dunia.
Mtakatifu Yohane Paulo II alifariki dunia tAprili  2 mwaka 2005, yaani miaka 15 iliyopita na kuacha ushuhuda wenye mvuto katika maisha ya binadamu.
Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu Mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatikani akitoa ushuhuda wa maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 15 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipofariki dunia ameeleza kuwa;
Hata leo hii, katika hofu, wasi wasi na taharuki ya kuenea kwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, bado Kanisa linaamini kuwa Mtakatifu huyo  anaendelea kuiombea dunia na watu wa Mungu katika  dhoruba hii kali.
Takwimu za maambukizi na vifo vinavyotokana na Virusi vya Corona inaonekana kuongezeka maradufu, kiasi cha kuwakatisha watu tamaa ya maisha. Watu wametikiswa kutoka katika undani wa maisha yao kiasi cha kuanza kukata tamaa.
Lakini Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mwamini hodari na shupavu katika maisha na utume wake.
Taa ya imani ilikuwa ni dira na mwongozo wa maisha yake, hata pale ilipoonekana yupo kwenye mahangaiko ya kuugua kwa muda mrefu, lakini bado aliendelea kuwa ni mtu mwenye amani, furaha na utulivu wa ndani.
 Ni mwamini ambaye alikuwa safarini kuelekea kwenye maisha na uzima wa milele.
Hiyo ni changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na fumbo la kifo katika maisha yao.
Ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mungu.
Hata baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mnamo Mei 13 mwaka 1981, Mtakatifu Yohane Paulo II aliendelea na maisha na utume wake katika hali ya utulivu na amani ya ndani.
Leo hii, watu wengi wamekosa imani na matumaini ya maisha na uzima wa milele.
 Matokeo yake wanaelemewa sana na simanzi na majonzi makubwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake; katika magumu na mahangaiko yake ya ndani, daima alikita maisha yake katika matumaini na akawataka waamini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na fumbo la kifo kwa imani na matumaini.
Mtakatifu Yohane Paulo II, aliweza kushuhudia yale yaliyokuwa yanamgusa kutoka katika undani wa maisha yake katika Waraka wake wa Kitume, “Mateso yanayookoa” “Salvific Dolores.”
Alisema kuwa, mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanapaswa kupata jibu makini kutoka katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu anayemfahamu fika mwanadamu katika mahangaiko yake.
Kardinali Angelo Comastri anasema, maadhimisho ya Fumbo la Pasaka kwa Mwaka 2020 yamegubikwa na taharuki ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa mwaka huu, hakutakuwa na maadhimisho ya hadhara na badala yake, waamini wanahamasishwa kufuatilia maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii. Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II kabla ya kifo chake, kutokana na kuelemewa na ugonjwa alilazimika kufuatilia maadhimisho haya akiwa chumbani mwake, hali ameshikilia Msalaba, akiwa na matumaini ya maisha na uzima wa milele baada ya kuhitimisha hija ya maisha yake hapa duniani.
Katika kipindi hiki cha taharuki na hofu kubwa ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, Baba Mtakatifu Fransisko anaendelea kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika sala, ibada, sadaka na majitoleo mbali mbali.
Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na ibada ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kristo Yesu, kabla ya kukata roho, alipenda kuwakabidhi wanafunzi wake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.
 Ndiyo maana Mama huyu alikuwa n anafasi ya pekee sana katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II.
Katika maisha kila mtu amekabidhiwa Msalaba wake, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Msalaba huu unakuwa ni chemchemi ya upendo na mwanga angavu wa maisha! Mtakatifu Yohane Paulo II ni kiongozi aliyeitupa mkono dunia akiwa na siri kubwa moyoni mwake.
 Hii ni siri ya mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanayokoa na kukomboa, changamoto kubwa hapa ni kuwapelekea wengine ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU