‘Wajibu wa serikali ni kuangalia Raia wake’



ASkofu wa Jimbo Katoliki  Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwe-Mugizi ameiomba serikali kusaidia baadhi ya vituo vinavyowasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye jamii.
 Askofu Niwe-Mugizi ameyasema hayo Machi 2 mwaka huu wakati akifungua bweni la wasichana katika kituo cha watoto cha Nazareti kilichoko Nyamiaga, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera. Hafla hiyo ilitanguliwa na tukio la kubariki vyumba vya bweni hilo.
“Watoto wanaosaidika ni wa jamii ya Tanzania na hivi hata serikali inapaswa kufikiria pia nini inachoweza kufanya ili kusaidia huduma ya hiki kituo ili kiendelee,” Baba Askofu NiweMugizi huku akiongeza;
 “Najua serikali ina mambo mengi sana lakini wakishaona kwamba kituo kinasaidia watoto wa Tanzania, wataweza kutuunga mkono. Inawasaidia hata wao kwa sababu ni wajibu wa kwanza wa serikali kuwahudumia hawa watoto.
Serikali ndiyo inastahili kuwa mstari wa mbele katika kuangalia mahitaji ya raia wake na haswa watoto maana ukishawaacha waishi maisha yasiyopendeza basi kesho unapata watoto wasio na maadili, walio wakorofi.”
 Aidha, amewahimiza wazazi wa watoto hao kushirikiana na Masista hao ili kuwatunza hawa watoto.
 “Wazazi wakifundishwa kwamba kufika hapa kituoni na kumsalimia mtoto kunajenga uhusiano ambao ni wa kibinadamu ni muhimu sana. Hata kama huna rasilimali za kumtunza, mtoto ataona kwamba unampenda,” ameeleza.
 Pia  amewahimiza watoto kuwa na nidhamu na kuwapenda walezi wao.
 Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika hilo Barani Afrika, Sista Christiane Lapierre ameshukuru Mungu kwa mafanikio hayo.
Ametaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo mojawapo ikiwa ni upungufu wa misaada kutoka kwa wafadhili na kupata wakati mgumu wa kuendesha kituo.
 “Tangu zamani tulitamani kupokea watoto wasichana, na sasa tumefanikiwa na ni furaha kubwa kwamba tumejenga nyumba yao ya kuishi.
Tunamshukuru Askofu Severine kwa kuja kubariki jengo hili. Asante kwa masista wote waliojitoa wakati wa ujenzi,” amesema =Sista Lapierre wakati wa hotuba yake.
 Mmoja wa watoto wanaolelewa kituoni hapo ambaye pia ni wanafunzi wa shule ya Msingi Nyamiaga Filbert Mugisha amesema watazidi kushirikiana na masista pamoja na wafanyakazi ili kufikia ndoto zao.
 Kituo cha Nazareti kinasimamiwa na Shirika la Masista wa Mtakatifu Christiana  linalofanya utume kwenye Jimbo Katoliki  Rulenge-Ngara. Kituo hicho kinatoa malezi kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu. 
 Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2012 huku kikipokea watoto wa kiume tu, lakini baada ya kuzindua jengo hilo, sasa kimeanza kupokea watoto wa kike wanatoka katika mazingira hatarishi.
Kwa sasa kituo hicho kinajumla ya watoto 39 kati yao wavulana ni 28 na wasichana 11 wote wakisoma shule za msingi ikiwemo shule za msingi za Nyamiaga, Mbinyange na Ngara mjini.
Pia wapo watoto 64 ambao wanasaidiwa wakiwa nje ya kituo yaani nyumbani kwao lakini pia wana watoto tisa ambao wanasoma shule za sekondari za Ndomba na Kabanga pamoja na mwanafunzi msichana mmoja ambaye anasoma QT katika shule ya sekondari ya Lukole.
 Kwa mujibu wa Askofu NiweMugizi, Jimbo la Rulenge-Ngara lina vituo viwili vya kuwasaidia watoto wanaotoka mazingira magumu. Kituo kimoja kinasimamiwa na Masista wa Shirika la Mtakatifu Francisko wa Bernadetta wa Lourdi, (FSSB). Kituo cha pili kinasimamiwa na Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresa wa Calcutta, (M.C) vyote vikiwa kata ya Rulenge.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU