Askofu Mhasi asimikwa Tunduru Masasi

Na Pascal Mwanache, Tunduru
ASKOFU Filbert Mhasi amewekwa wakfu na kusimikwa kuwa wa Askofu wa nne wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi, katika adhimisho la MisaTakatifu lililofanyika katika Kanisa Kuu la Mtalatifu Fransisko Xavery na kushuhudiwa na mamia ya waamini.
Akimkaribisha Askofu Mhasi katika urika wa maaskofu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema kuwa Kanisa jimboni humo na Taifa kwa ujumla halina budi kuishi katika misingi ya kufanya kazi pamoja kama familia moja yenye mshikamano na dira ya kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha Mhashamu Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Askofu Mkuu Mteule wa Jimbo Kuu teule la Mbeya ametoa rai kwa waamini wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi kushikamana na mchungaji wao mkuu na kudhihirisha tunu za familia yenye kushirikiana kwa ajili ya ustawi wao.
“Ninatoa rai kwenu kuishi kwa mshikamo,mapendo na umoja ndani ya jimbo lenu. Mshikamane na askofu wenu mpya. Mdhihirishe maisha ya familia inayoishi kiaminifu na mshikamo wa dhati kati ya wazazi na wanafamilia. Waamini wajione wana baba ambaye ni kimbilio na mtetezi wao, na baba ajione ana wanafamilia watakaomfariji na kumtia moyo katika utume wake. Na hivyo hata taifa zima liishi katika misingi hiyo ya kufanya kazi kwa pamoja” ameeleza Askofu Nyaisonga.
Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametoa pongeza kwa maaskofu watangulizi wa Askofu Mhasi na kusema kuwa wameweza kuwajenga watanzania kiroho, huku akitoa wito kwa waamini jimboni humo washikamane na askofu mpya na kumtii.
Aidha Prof. Kabudi ameliomba Kanisa Katoliki liendelee kujenga jamii yenye maadili mema hasa kwa vijana ili hatimaye wajiepushe na matumizi ya dawa za kulevya, kukaa vijiweni bila kazi na kuishia katika michezo ya kamari.
“Kwa miaka mingi Kanisa Katoliki nchini limetoa mchango wake wa  kiroho, kiuchumi na kijamii katika taifa letu. Baadhi ya sekta ni pamoja na elimu, afya, kuwahudumia walemavu, wazee, na kuwajenga watanzania kimaadili. Endeleeni kuwalea vijana wetu kimaadili, wasijiingizekwenye matumizi ya madawa ya kulevya, wachape kazi na kutoishia katika michezo ya kamari” amesema.

Kwa nini Tunduru na siyo Masasi?
Kwa upande wake kiongozi wa Misa hiyo ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mhasi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema kuwa makao makuu ya Jimbo Katoliki Tunduru Masasi yamewekwa Tunduru kwa sababu alipofika Tunduru aligundua tatizo la msingi la watu wengi kutoipokea imani ya Kanisa Katoliki.
“Siri ya ndani kuhusu neno hilo, nilipofika hapa Tunduru kwa mara ya kwanza siku ya jumamosi,  kesho yake nikakuta vijana wawili tukasalimiana vizuri kisha nikawauliza hivi ndugu zangu mmesali wapi leo? Wakaniambia wao ni wayao. Mwanzoni sikuelewa maana yake, Padri aliyenisindikiza akasema walitaka kukuambia kuwa wao ni waislamu. Nikagundua kuna tatizo la msingi siyo tu la kidini bali pia la kiutu” ameeleza Kardinali Pengo.
Pia ameongeza huko jambo hilo ndilo lililompa hamasa ya kwa nini myao asiwe mkatoliki, na hivyo  wakati huo aliamua kwa dhati kwamba kama Papa akimruhusu makao yake yangekuwa Tunduru.  “..na mimi nitakwenda kuhesabiwa kama yao” amesema.
Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Filbert Mhasi imefanyika Februali 17 na kuhudhuriwa na waamini toka ndani na nje ya Jimbo Katoliki Tunduru Masasi akiwemo pia Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu Benjamin Mkapa na mke wake Mama Anna Mkapa.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI