Sera za nchi zisipingane na mpango wa Mungu-Ask. Dallu
WATUNGA
sera mbalimbali za nchi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa upendo na kwa
kuwahusisha wadau wa sekta husika ili sera hizo sizipingane na mpango wa Mungu
kwa watu wake.
Rai hiyo
imetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu
wakati akitoa homilia yake katika Ibada ya masifu ya jioni yaliyotangulia
kusimikwa na kuwekwa wakfu Askofu Filbert Mhasi wa Jimbo Katoliki Tunduru
Masasi.
Askofu Dallu
amesema kuwa Kanisa linaendelea kusali na kushukuru kwa hatua zile
zinazochukuliwa na kuona kama kweli hakuna sheria zinazokuwa kinzani kwa nafasi
ya Kanisa ya kutoa huduma mbalimbali nchini.
“Tunaendelea
kusali kwa ajili ya vituo vyetu vya kutoa malezi ya kuelekea katika huduma ya
upadri na nyumba za kitawa. Naomba huko tusikanyage kanyage katika miundombinu
ya hawa wanaoandaliwa kuwa mapadri. Wasipewe idadi tofauti na mwongozo wa
kawaida wakaonekana wao wawe darasa la wanafunzi 25 tu, hapana. Hiyo siyo kazi
ya kikundi wala mtu, wito ni wa Mungu anaita anavyotaka. Mungu hawezi
akatulazimisha katika wito wetu” ameeleza Askofu Dallu.
Aidha ametoa
wito kwa wale wote wanaotunga sheria wajawe na moyo wa upendo na kuleta hali
ile ambayo imekuwa nguzo kubwa Kanisa Katoliki Tanzania.
“Tusali
tumuombe Mungu shule zetu ambazo zinalea kuelekea kuanza kidato cha kwanza basi
wapate nafasi ya kulelewa hapo ili tuwaandae. Tusiweke tu miongozo ambayo
itakuwa inatufuta bila hata wadau wenyewe kuzungumza. Hebu fikiria kwa Kanisa
la Tanzania nafasi alipo Askofu Mkuu Protase Rugambwa. Yeye ni mtanzania na
aliundwa kwa miundombinu hii tuliyonayo Tanzania. Tunaomba tuendelee
kuiimarisha miundombinu hiyo na kuikaza zaidi siyo tu kwa ajili ya Kanisa, bali
upatikanaji wa elimu bora katika nchi yetu” amesisitiza.
Pia Askofu
Dallu ametaka kuimarishwa kwa malezi ya mapadri kwa kusema kuwa malezi ya
upadri hayapaswi kuwa ya mkato, na kwamba lazima mapadri walelewe kwa muda wa
kutosha.
“Upadri siyo
haki ni wito, ni upendo wa Kristo mwenyewe anatushirikisha kwa upendeleo, siyo
haki. Upadri ni wa dunia nzima” ameongeza.
Comments
Post a Comment