Mamia wamzika Padri Mwechibindu
Mamia ya waamini kutoka Parokia
mbalimbali za Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, mapadri, watawa na maaskofu
kutoka majimbo mbalimbali nchini na viongozi mbalimbali wa serikali wamejitokeza kumzika marehemu Padri Andrew Mwachibindu
aliyefariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili usiku wa January 12, 2019.
Akiongoza Ibada ya Misa Takatifu
ya kumwombea marehemu kabla ya mazishi yake yaliyofanyika katika Kituo cha
wafia dini Pugu Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
Mhashamu Yuda Thadei Ruwaichi amemtaja marehemu kama mtu aliyekuwa mtulivu,
mwenye nidhamu na mipango chanya ya utumishi.
Aliyeongozwa na uchaji wa kimungu
na mchungaji msikivu aliyependa kufanya yote vema.
Amesema katika maisha mwanadamu
anapitia magumu na mateso mazito na anapokabiliwa na mateso hayo huwa anakuwa
na hofu hivyo kila mwanadamu anapaswa aongozwe kwa imani yake kwa Kristo
anapokabiliwa na kifo.
Ameongeza kuwa wakristo wote
hawanabudi kuishi kama wana wa Mungu kwa kumuangaza Kristo katika maisha yao
yote hapa duniani bila kusahau kukumbushana na kuhimizana kumwongokea Mungu.
“Ayubu alipata mateso na
mahangaiko mengi sana kupitia hayo alipata ushauri mwingi kutoka kwa watu
waliodhani pengine ushauri wao ungeweza kufanya aondokanae na mateso
lakini Ayubu alishikilia imani ya
kumpenda Mungu katika mahangaiko yake yote” amesema.
Pia ameongeza kuwa kwa namna hiyo
ya mateso aliyoyapitia Ayubu bila kuwa na mashaka na Mungu viyo hivyo na kila
mwanadamu atambue kwamba uhai wa binadamu ni mali ya Mungu na kwa namna ya
pekee amshukuru Mungu.
Askofu Ruwaichi amewatahadharisha
watu ambao huwaondolea uhai wenzao wakisema wanawaonea huruma wasiteseke katika
mateso yanayowakabili na kusema kwamba mtu wa Mungu ni lazima ateseke hivyo
wanaofanya hivyo pengine hawamjui vizuri Kristo.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesikitishwa na kifo cha Padri Andrew
Mwechibindu akisema kwamba alipokea taarifa za kifo akiwa nchini India na alimwomba
Mungu amsaidie aweze kufika siku ya mazishi na Mungu amemsaidia kufika katika
mazishi hayo.
Ameongeza kuwa kwa nyakati
tofauti alimpeleka marehemu katika Parokia ya Mafia akidhani angeweza kupumzika
kulingana na hali ya upepo wa huko lakini ikawa tofauti kwake. Mwadhama pia
ametoa pole kwa wazazi, ndugu, jamaa, mapadri na watawa wote wa jimbo hilo kwa
msiba huo mzito.
Kwa upande wake kaka wa marehemu
Ndugu John Simon Mwechibindu amemshukuru Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
Maaskofu wote wa Jimbo Kuu Dar es salaam, mapadri na kwa namna ya pekee
walivyofanya kazi ya utume pamoja na marehemu Padri Andrew Mwechibindu na
kusema kwamba Kanisa limepata pigo kubwa sanjari na familia yao kwa sababu ni
muda mfupi wamewapoteza dada zao wawili kwa hiyo kufariki kwa padri Mwechibindu
ni pigo la pili.
Marehemu Padri Andrew
Mwechibindu ambaye alizaliwa January 02,
mwaka 1965 akiwa ni mtoto wa tatu kati ya watoto nane wa familia ya mzee
Mwachibindu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo yaliyosababisha ashindwe kufanya
kazi.
Akiwa hai amehudumia parokia mbalimbali
zikiwemo Mburahati, Magomeni, Mafia, Mikocheni, Mbezi Beach na mpaka mauti
yanamkuta alikuwa katika parokia ya Mikocheni alipokuwa akisubiri kuhamia
katika Parokia ya Mwanagati kama Paroko.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na
Raisi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Gervas Nyaisonga wa
Jimbo Kuu Teule Mbeya, Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki
Mtwara, Askofu Yuda Thadei Rwaichi Mwadhama Polycarp Kadinari Pengo na
Monsinyori Deogratias Mbiku .
Comments
Post a Comment