Maaskofu Katoliki Tanzania wapewa mafunzo juu ya Uongozi Bora
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) kwa ushirikiano na Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki AMECEA
na Missio, wametoa mafunzo kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki juu ya uongozi Bora.
Mafunzo
hayo ya siku tano yamefanyika kuanzia
Januari 14-19, mwaka huu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Kurasini jijini Dar es Salaam.
Maaskofu hao
wanajengewa uwezo juu ya Uongozi na
Usimamizi wa taasisi, Uongozi Endelevu; Umoja wa Kanisa Katoliki pamoja
na Ushauri na Usimamizi.
Awali Katibu
Mkuu wa AMECEA Padri Anthony Makunde ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni ya awamu ya
pili ambapo awamu ya kwanza yalikuwa
yanafadhiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani sasa awamu ya pili
yanafadhiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kupitia shirika lao la
Missio.
Aidha
ameeleza kuwa alifanya safari na Rais wa
AMECEA Mhashamu Charles Kasonde kwenda kukutana na Rais wa Missio Aachen,
Makamu wake na Afisa wa Ushirikiano wa
Kimataifa ili kujitambulisha lakini pia kuendeleza awamu ya pili ya mafunzo kwa
maaskofu na wasaidizi wa karibu wa maaskofu katika ukanda wa AMECEA pamoja na
miradi mingine inayotekelezwa na AMECEA kwa kufadhiliwa na Missio.
“Ndiyo maana
tupo hapa timu ya AMECEA tukishirikiana na TEC ili kufanikisha mafunzo haya ya
siku tano,” ameeleza Padri Makunde.
Aidha
ameeleza kuwa, amepewa wajibu wa kuwakumbusha maaskofu wote kuhusu mafanikio ya
AMECEA tangu ilipoanzishwa miaka 58 iliyopita.
“Tunajivunia
kwa kutembea pamoja hadi sasa tumefikisha miaka 58 tukiwa na ongezeko la
waamini wabatizwa katika ukanda huu wa AMECEA.
AMECEA imezaa
Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, Chuo cha AMECEA cha Kichungaji na Chuo cha
Mwenyeheri Bakanja.
Kumekuwa na
ongezeko la jumuiya ndogondogo pamoja na mashirika ya kitawa kwa wanawake na
wanaume,” amesisitiza.
Amewataka
Maaskofu kutathmini maono ya waanzilishi wa AMECEA ambao walitaka kutembea
pamoja kwa kuwa na mbinu na mikakati ya pamoja ya kichungaji.
Kumbe ilikuwa
ni ari ya waasisi wa AMECEA kuwa na umoja na ushirikiano kwa ajili ya maendeleo
ya ukanda wa AMECEA.
Pia kuna
ongezeko la Maaskofu, majimbo na mapadri katika ukanda wa AMECEA.
Hivyo
maaskofu wanapaswa kuimarisha maono hayo ya waasisi hususani mada saba za
mkutano Mkuu wa Kwanza wa AMECEA Julai 1961.
Katika
mkutano huo Mkuu wa kwanza wa AMECEA, baadhi ya mada zilikuwa ;Kanisa na Vyombo
vya habari kwamba Maaskofu waanzishe kituo cha televisheni cha AMECEA, radio ya
AMECEA na kiwanda cha uchapichaji cha ukanda huo.
Pawe na kituo
cha kutoa malezi ya kiroho kwa mapadri wa jimbo, Chuo Kikuu cha Ukanda
ambapo tayari kipo chuo Kikuu cha Afrika Mashariki CUEA,
masuala mbalimbbali ya haki na amani nk.
Huku
wakiendelea kutathmini hayo wanapaswa kujua kuwa, ingawa AMECEA ina mafanikio
bado kuna changamoto mbalimbali zinazopaswa kutatuliwa kwa ajili ya maendeleo
ya nchi wanachama wa AMECEA.
Aidha
wakumbuke kuwa, wafadhli wamepungua hivyo maaskofu wanapaswa kuwa na mbinu za
kujitegemea ili asilimia kubwa ya mapato yao yatokane na mapato ya ndani badala
ya nje.
Ndiyo maana
Missio kwa kushirikiana na AMECEA na TEC wanatoa mafunzo hayo yakini ili
maaskofu wapate ujuzi na mbinu za kubuni
miradi ya kujitegemea ikiwemo kubuni miradi endelevu.
Kwa upande
wake Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Dkt. Charles
Kitima amesema kuwa, mkutano huo unakuja wakati Kanisa linapaswa kupata mbinu
na ujuzi wa kumiliki rasilimali watu, fedha
nk. ambazo ni endelevu.
Ametaka washiriki watathmini ni kwa jinsi gani wana
mikakati endelevu ya Usimamizi wa taasisi, Uongozi Endelevu; Umoja wa Kanisa
Katoliki, Ushauri na Usimamizi.
“Hatuwezi pia kufanikiwa katika hayo bila ya
kuwa na umoja na mshikamano. Mafanikio
ni kuwa na uongozi bora unaotoa miongozo yenye tija na ushirikiano na mikakati
endelevu ya maendeleo,” amesema Padri Kitima.
Comments
Post a Comment