Wanaosimamia watoto katika ubatizo wawe waamini waliokomaa kiimani-Ask. Rwoma
Mapadri, wazazi na viongozi wa Kanisa wametakiwa kuwa makini
kuwachagua wasimamizi wenye uelewa na Imani, na kuwaonyesha njia wale wote
wanaowasimamia watoto katika Sakramenti
mbali mbali za Kanisa Katoliki.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu
Desderius Rwoma katika homilia yake wakati wa Misa Takatifu ya somo wa Parokia
ya Mt. John Bosco katika Parokia ya Mt. Yohani Bosco - Kamishango Jimboni humo.
Katika homilia yake Askofu Rwoma amesema kuwa, ni vizuri wazazi
wakawachagulia watoto wao wasimamizi wenye sifa na waliokomaa kiimani katika
Sakramenti za ubatizo na kipaimara.
''Katika Sakramenti za Kanisa kuna mtu anaitwa msimamizi, sasa
sifa kuu ya msimamizi ni kumuonyesha njia yule unayemsimamia, mzazi anapaswa
kuwa kiongozi kwa yule unaye msimamia na kiasi cha maisha anayoishi unaweza
kusema huyu anaweza kuwa mtu mwema sio kuokota okota tu mtaani.
Aidha, anayekuwa msimamizi lazima amjue vyema anayemsimamia
ili kumshauri asije akapotea njia na kuingia kusiko faa, sasa unadhani
msimamizi akiwa mlevi muda wote yupo kwenye pombe ataweza kumshauri na kumkea
aliyepokea sakramenti,'' amesema Askofu Rwoma.
Aidha Askofu Rwoma amewataka Wakristo wakatoliki kuzitumia
vizuri karama za upendo na huruma walizopewa na Mungu, na kuzionyesha kwa
wengine, na kutanguliza karama ya sala kuwa kipaumbele kwa kila
jambo.
''Karama ya huruma na upendo kila mmoja amepewa, onyesheni
karama hizo kwa wengine pamoja na karama ya sala ambayo ni karama za kila mtu.
Kila mmoja anatakiwa kusali yeye na familia yake na kusali
pamoja na wengine, hivyo ni vizuri mkazionyesha karama hizo na kuwashirirkisha
wengine na tutangulize kilicho cha kwanza ambayo ni sala, '' amesema Askofu
Rwoma.
Pia amezitka jumuiya ndogo ndogo kusali pamoja ili kujiiimarisha
kiroho katika kutafuta utakatifu na kuwa marafiki kwa wakosefu ili
kuwarudisha katika njia inayofaa kama alivyofanya Mt. Yohani Bosco na kusaidiana
katika shida mbali mbali.
Katika Misa hiyo Takatifu, Askofu Rwoma wametoa Sakramenti ya
ubatizo kwa watoto zaidi ya 325 na kusimika jumuiya ndogo ndogo zaidi ya 70,
amewabariki waamini waliorudi katika sakramenti mbali mbali za Kanisa pamoja na
kuwaapisha viongozi wa vyama vya kitume, jumuiya ndogo ndogo na viongozi wa
Halmashauri ya Parokia..
Comments
Post a Comment