Uhai wa Kanisa si wingi wa mapadri, waamini, watawa

Askofu wa Jimbo Katoliki Tunduru Masasi Mhashamu Askofu Filbert Felician Mhasi amewakumbusha waamini kuwa uhai wa Kanisa siyo wingi wa waamini makanisani, waseminaristi maseminarini, watawa katika nyumba za kitawa bali ni maisha yao ya Imani wanayoyaishi.
Rai hiyo  ameitoa hivi karibuni akiongoza Misa Takatifu  katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Mtume Kipalapala Tabora akitoa huduma ya usomaji Masomo kanisani na huduma altareni kwa mafrateri wa mwaka wa pili na watatu.
Askofu huyo amesema uhai wa Kanisa hautegemei wingi wa mafrateri katika seminari na swali muhimu ni  Je, wanastahili?
Aidha Askofu Mhasi amesema Upadri unajengwa katika maisha imara ya Ukristo, tunakuwa wakristo kabla ya kuwa mapadri hivyo ni wajibu  wa kila mkristo kuishi imani yake kwa uaminifu. Amewakumbusha mafrateri hao kuwa mabalozi kule waendako baada ya kuwa mapadri.
Maisha ya Upadri ni sawa na mbio za kijiti, watu tunapasiana kila mmoja kwa wakati wake na stamina yake, ni vema zamu yako ikifika ukimbie haraka ili Injili isije ikafia mikononi mwako, tumia karama zako na nguvu zako kukimbiza Injili ya Kristo kwa haraka.
Kila Mseminaristi anapaswa kujivunia nafasi ya kwanza ya kuwa mkristo na kuishi Ukristo, “mafrateri jiepusheni na tamaa ya vyeo kanisani, ridhika na nafasi ya kwanza ya kuwa mbatizwa uwe mkristo na uishi ukristo, ndiyo upadri na Uaskofu utafuata.
 Acheni kujiwekea matarajio makubwa kanisani mtaishia kuchanganyikiwa bure,” Askofu amesema.
Aidha Askofu Mhasi amesema mara baada ya Kristo Yesu kumaliza utume wake wa kimwili duniani aliacha sera ya kwenda kuhubiri Injili ulimwenguni pote mpaka ukamilifu wa dahari, hiyo ndiyo kazi ya upadri mnayoiendea, nendeni mkawe alama ya uwepo wa Mungu ndani yenu.
Amesema waseminaristi hawana budi kuwa wasikifu kwa walezi wao ili baada ya malezi wawe mapadri wema na watakatifu.
Mseminaristi au frateri hapaswi kuwa na haraka ya kupewa daraja ya upadri, vyote hutolewa na Mungu kwa wakati anaoona unafaa.
Aidha Askofu huyo amesema Mungu ndiye anayeita, anayechagua kuwa chombo chake kwa wakati wake, katika mazingira anayotaka yeye , hata kwa macho yetu ya kibinadamu kama tunayaona hovyo, akitaja wito na tabia ya Mtume Paulo aliyekuwa na kibali cha kuua lakini Mungu alimwita na kumtumia.

Mwisho Askofu Mhasi amewaasa mafrateri wote kutumia muda wao vizuri wawapo seminarini ili baada ya malezi wakawe wahudumu wazuri na bora wa Kristo na si bora mapadri na kuwaomba wakae mbali na tamaa ya vitu na malimwengu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU