Ndoa hazijengwi kwa pesa, mali -Ask Kinyaiya


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki  Dodoma Mhashamu Beautus Kinyaiya, amesema baadhi ya wanaume wengi hufikiri na kudhani kwamba kuwa na Pesa nyingi ndio unaweza kuwa na ndoa imara .
Askofu Kinyaiya amesema hayo hivi karibuni, wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya kubariki ndoa tatu na kutoa Sakramenti Takatifu ya Ubatizo na Kipaimara, katika Parokia ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola Miyuji Kusini Jimbo Kuu Katoliki Dodoma. 
Amesema kuwa, kuna wanaume wengi wenye pesa na uwezo mkubwa wa kiuchumi lakini ndoa zao zimevunjika, hivyo wanapaswa kutambua kwamba ndoa si kuwa na pesa nyingi bali ni kupendana na kuheshimiana. 
“Nahilo wanaume wengi sana huwa wanasahau anafikiri akiwa na hela sana mwanamke yoyote anaweza kuwa mke wake. Hapana kuna wenyepesa nyingi sana lakini wameachwa, hawakukubalika au wameachwa.
 Pesa sio kila kitu kuna vitu vya ziada ambavyo anatazama ndani yako anavyoviona na kukubali ulivyo,” amesema Askofu Kinyaiya.
Aidha amesema kwamba,  baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia dhana ya mwanaume ni kichwa cha familia kuwanyanyasa wake zao, huku akiwataka wanandoa wote nchini kukiendeleza kile ambacho mke alikipenda kutoka kwa mume na mume alikipenda kutoka kwa mke wakati wa uchumba wao. 
“Kile ambacho mwenzako alikupendea tafadhali endelea kukipalilia, usiseme ameshanioa kwahiyo basi nakaakaa tu, inaletaga matatizo kwenye ndoa vile ambavyo vitu alivyovipenda kama havioni tena matatizo yanaanza.
Nawaombeni sana kila mmojawenu kile ambacho mwenzako alikupendea kishindilie kiendeleze narudia,” amesema Askofu Kinyaiya.
Aidha amewatahadharisha juu lugha wanayoitumia daima ionyeshe mshikamano na umoja wao kwani kila walichonacho katika familia ni cha kwao wote na si cha upande mmoja. 

Aidha  amesema kuwa, katika maisha ya watu wawili na zaidi  kuna mambo ambayo lazima watakorofishana, hivyo jambo  la kwanza wanalopaswa kufanya ni kupenda kila mmoja kutoa sadaka,  huku akisema wanaume wengi wamekuwa wagumu sana wa kuomba msamaha. 
“Na kingine muhimu sana ni kusameheana kwasababu katika maisha hapa na pale lazima mkorofishane mpo watu wawili na tabia tofauti mahali flani lazima mtapishana.
Kwahiyo suala la kwanza mpende kila mmoja kutoa sadaka, mambo flani lazima usamehe, lazima katika maisha ili mwenzako asamehe mambo yaende,” amesema Askofu Kinyaiya.
Amesema kuwa, wito wa ndoa ni maisha si ya kubadili mke au mume kama usafiri au kazi,  huku akawataka wanandoa kuchunguzana kabla ya kuandikisha na kufunga ndoa yao,  kwani kumekuwa na migogoro mingi inayosababisha ndoa nyingi kuvunjika. 
“hilo ni muhimu sana ndugu zangu na hasa vijana mlioko ndani humu kwasababu tunaishi karne ambayo watu wanapenda sana wanaishi kitu flani akikichoka anataka kubadili, mtu ananunua redio akishaichoka leta nyingine, mtu ananunua bodaboda anakaendesha ikija mpya uza nunua nyingine, hata kazi tunabadili sana kaa miaka mitano kazini nataka kubadili.
Sasa na mke mnafanya hivohivo hapana, ndoa ni ya maisha na ndiyo maana huwa tunapenda wanandoa wachunguzane mda wa kutosha,” amesema.
Askofu Mkuu Kinyaiya amehitimisha kwa kuwaasa wanandoa wote kwamba, mali wanazozipata katika ndoa yao zisiwafanye kutokuelewana bali waendelee kushikamana hata katika changamoto mbalimbali za maisha. 

Misa hiyo takatifu ya kubariki ndoa imeenda sambamba na utoaji wa sakramenti ya kipaimara kwa wanandoa watatu ambao walikuwa bado hawajaimarishwa kwa sakramenti hiyo, sanjari na kubatiza watoto wawili Sara na Grece.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU