Msitumie vibaya utajiri wenu -Askofu Kinyaiya asema
Na Ndahani Lugunya na Rodrick
Minja, Dodoma
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya, amekemea tabia ya baadhi ya wakristo waliopewa
utajiri na Mwenyezi Mungu kuutumia vibaya utajiri huo hususani kwa kuwanyanyasa
wanyonge, yatima, masikini na wasiojiweza.
Ameyasema hayo wakati akitoa
homilia yake kwenye adhimisho la sadaka ya Misa Takatifu, katika Parokia ya
Bikira Maria Mama wa Damu Azizi ya Yesu-Kisasa Jimboni Dodoma, Misa iliyokwenda
sambamba na utoaji wa sakramenti Takatifu ya kipaimara kwa vijana 76 wa Parokia
hiyo.
Katika homilia yake Askofu
Kinyaiya amesema kuna baadhi ya wakristo wamejaliwa kupata utajiri kwa halali
kabisa, lakini kosa linakuja pale mtu anapoutumia utajiri huo kwa ubadhilifu na
kuzitumia katika matumizi yake ya kila siku pasi na mpangilio mzuri.
“Mmejaliwa utajiri na Mwenyezi
Mungu hivyo utumieni kwa kutenda mema na sio kunyanyasa wengine ambao
hawakujaliwa utajiri huo kwani hata ipo siku mwenyezi munghu anaweza
kukunyang`anya utajiri huo pasi kujua lolote lile” aliongeza Askofu Mkuu
Kinyaiya
Katika hatua
nyingine Askofu Kinyaiya amewataka wazazi na walezi wenye watoto
kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi miaka saba, kuanza kuwajengea msingi wa kuwafundisha
lugha ya kiingereza kabla ya kuwapeleka shuleni kuanza elimu ya msingi.
Amesema kwamba, umri wa mtoto
kuanzia miaka hiyo akili yake ni kama sponji mpya ambapo huwa ni mwepesi wa
kufyonza kila kitu kwenye akili yake, kumbe wazazi wenye watoto wa umri huo
wawafundishe lugha ya kingereza kabla hawajawapeleka shuleni.
“Kwahio sasa wazazi
wenye watoto wadogo, umri wa kumsaidia mtoto ni pale anapokuwa kuanzia mwaka wa
kwanza mpaka wasaba akili yake kama sponchi mpya inayofyonza kila kitu, na ndio
maana watoto wanakuwa wepesi sana ukimnyima kitabu ataokota hata karatasi
njiani atasoma, akili ina dai ina uwezo mkubwa,’ amesema.
Amesema moja ya tatizo lililopo
nchini kwa watoto kutokufanya vizuri katika elimu ya sekondari ni lugha ya
kingereza, kwani wanapokuwa katika elimu ya msingi wanafundishwa masomo yao kwa
kutumia lugha ya Kiswahili, hivyo wanapofika ngazi ya sekondari lugha ya
kiingereza inawapa shida.
Sasa wazazi tunawasaidiaje katika
hilo, kama tumeshajua ile miaka saba ndio mahali pazuri kwa mtoto kufyonza,
wazazi muanze kusaidia watoto wakiwa nyumbani bado kwenye suala la lugha,”
amesema Askofu Mkuu Kinyaiya.
Ameongeza na kusema
kwamba wazazi wasisubiri tu watoto wakafundishwe lugha ya kingereza
wakiwa shuleni, wakati wapo watu wa karibu nyumbani wanaoweza kuwafundisha
lugha hiyo wakiwa hapo, ambapo amesema kama yupo Baba, Mama, Kaka au Dada
anaejua kingereza basi awajibike kumfundisha mtoto.
Katika hatua nyingine amewataka
vijana walioimarishwa kwa sakramenti ya Kipaimara na vijana
wengine nchini, kujiepusha na makundi mabaya yanayojihusisha na
utumiaji wa bangi na madawa mengine ya kulevya.
Amesema mazingira mtu anayoishi
wakati mwingine yanaweza kumfanya mtu akawa hovyo asipokuwa mwangalifu, hivyo
akawataka vijana kujitahadharisha na marafiki wanaoweza kuwashawishi kutumia
madawa ya kulevya.
Amewataka waimarishwa hao
kusimama imara katika kuitetea imani ya Kanisa Katoliki popote pale wanapkuwa,
kwani tayari wamekwishakuwa watu wazima kiimani.
Ibada hiyo ya Misa Takatif imekwenda
sambamba na zoezi la kubariki jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa la parokia
hiyo, ambapo ujenzi huo umefikia hatua ya kunyanyua nondo na umekwisha gharimu
takribani milioni 200 mpaka sasa.
Comments
Post a Comment