Jubilei miaka 75 Masista wa Upendo
‘Mkiushinda ubinafsi mtafanikiwa’
Na
Pascal Mwanache, Mbingu
MASISTA
wa Shirika la Upendo wa Mt. Fransisko Mahenge wameaswa kufanya kazi kwa
kushirikiana huku wakiweka kando ubinafsi ili kazi zao ziendelee kumtukuza Mungu.
Hayo yameelezwa na Askofu
wa Jimbo Katoliki Tundu-Masasi Mhashamu Filbert Mhasi katika Misa Takatifu ya
kuwakumbuka marehemu waanzilishi wa shirika hilo la masista pamoja na masista
waliofariki, ikiwa ni sehemu ya sherehe ya jubilei ya miaka 75 ya shirika la
masista wa upendo wa Mt. Fransisko Mahenge.
Akitoa homilia katika
misa hiyo Askofu Mhasi amewaasa masista hao kutotafuta mtetezi mwingine zaidi
ya Mungu pale wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali katika utume wao, bali
wadumu katika uthabiti wa imani yao na Mungu atawatetea.
“Inatupasa kumshukuru
Mungu kwa imani tuliyojaliwa kupitia Kristo. Waanzilishi wa shirika hili
walipigana vita vizuri na waliamini kuwa kuna maisha baada ya kifo. Ndiyo maana
wakawa imara katika imani yao. Hawakuwa wabinafsi, nanyi hamna budi kufanya
kazi kama timu huku mkiweka ubinafsi pembeni” ameeleza Askofu Mhasi.
Kwa upande wake Askofu wa
Jimbo Katoliki Ifakara Mhashamu Salutaris Libena amewataka masista hao
kuendelea na jitihada za kumkomboa mwanadamu kimwili na kiroho kama
walivyofanya watangulizi wao.
Ameyasema hayo katika
adhimisho la Misa Takatifu ya kutangaza injili iliyofanyika Oktoba 3, 2019
kuelekea kilele cha jubilei ya miaka 75 ya Shirika la Masista wa Upendo wa Mt.
Fransisko Mahenge.
Akitoa homilia katika
misa hiyo Askofu Libena amewaomba watawa hao kuendelea kuhubiri kwa maisha na
matendo yao kwa kumkomboa mwanadamu mzima kiroho na kimwili kupitia utume na
huduma mbalimbali za kijamii.
“Mfanye yale ambayo wale
waliokuja kutangaza Injili waliyafanya. Imani tuliyoirithi kutoka kwao
tuirithishe kwa wengine ili wamjue Mungu kwani dunia ina kiu ya neno la Mungu.
Wengi bado hawajamjua Mungu hivyo twende tukawainjilishe” ameeleza Askofu
Libena.
Kardinali
Pengo aagwa na kupongezwa Ifakara
Awali katika hatua
nyingine waamini wa Jimbo Katoliki Ifakara wameungana katika adhimisho la Misa
Takatifu kwa ajili ya kumpongeza Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kutimiza
miaka 75 ya kuzaliwa.
Akitoa neno la shukrani
katika misa hiyo Kardinali Pengo ameeleza kuwa amefurahi kuona jimbo hilo
halijadumaa bali linaendelea kukomaa.
“Jimbo la Dar es salaam
limezaa jimbo la Mahenge na Jimbo la Mahenge limezaa jimbo hili la Ifakara. Kwa
hiyo ninafurahi kuwaona wana Ifakara ambao ni wajukuu wa jimbo la Dar es
salaam. Nafurahi mmebaki wema na hamjadumaa” ameeleza.
Shirika la Masista wa
Upendo wa Mt. Fransisko wa Asizi lilianzishwa Juni 8, 1941 na Askofu Mkuu Edgar
Maranta OFMCap katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam. Wakati huo jimbo la
Mahenge lilikuwa sehemu ya Jimbo Kuu la Dar es salaam ambapo wakati huo Askofu
Mkuu Maranta alikuwa Askofu Mkuu wa Dar es salaam.
Idadi ya wanashirika
iliyopo sasa ni 334 ambapo masista wenye nadhiri mi 268 na walelewa wapatao 66.
Comments
Post a Comment