Jamii yatakiwa kuthamini wazee
Jamii imetakiwa
kuacha tabia ya kuwatelekeza wazee na kuwaacha waishi katika mazingira magumu.
Kauli hiyo
imetolewa na wazee walioshiriki kongamano la wazee katika kuadhimisha siku ya
wazee duniani ambapo kitaifa imefanyika mkoani Mtwara na kuhudhuliwa na
wawakilishi wa wazee kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Wazee hao
wamedai kuwa kwa sasa wengi wao wanaishi maisha magumu sana kutokana na vijana
wao waliowasomesha kwa shida na taabu leo wanawaona mizigo na wanashindwa
kuwasaidia.
“Baadhi ya
watoto wetu wanatuona kama mizigo maana hatuna nguvu tunawategemea kwa kila
kitu.
Pia
wanasahau kutimiza wajibu wao wa kulea wazazi wao kama sisi tulivyotimiza wajibu wetu
kuwalea na kuwasomesha.
Hivyo
wanaposahau kuwa nasi pia tuliwalea na kuwapa elimu, wanajiona kuwa mafanikio wanayopata ni kutokana na juhudi zao
tu.
Inasikitisha
kuona wazee wanaishi maisha magumu sana
kwa kuwa watoto wao wanawaona kuwa ni mizigo isiyobebeka”amesema Mzee Mohamedi
Selemani.
Miongoni mwa
changamoto ambazo zinawakabili wazee kwa sasa katika maeneo mengi ni pamoja na
huduma za afya,ambapo wameiomba serikali kuendelea kuboresha sera ya afya
ambapo itakuwa msaada kwa wazee ambao walitumia muda na nguvu zao katika
kulitumikia taifa.
Pia wazee
wametakiwa kushikamana ili kujikwamua katika uzee wao ambapo ni umoja wao pekee
ndio utasaidia kufikisha vilio vyao kwa serikali na jamii kwa ujumla maana bado
kuna kundi kubwa la wazee ambao wameendelea kuwa nje ya umoja hali ambayo
inachangia kushindwa kujua changamoto zinazowakabili.
Aidha pia
vijana na viongozi katika nafasi mbalimbali wametakiwa kuwakumbuka na kuwajali
wazee kwa kuwa wao ni sehemu muhimu ya ustawi wa taifa na maisha ya watanzania
na wamekuwa historia katika harakati mbalimbali za uhuru na maendeleo ya taifa.
Wanapozeeka jamii inayo wajibu wa kuwaenzi kwa
kazi zao zilizotukuka.
Akifungua
kongamano la wazee kitaifa lililofanyika
katika ukumbi wa Benki Kuu Kanda ya Kusini Mtwara, Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dakta John
Jingu, amedai kuwa chimbuko la siku ya wazee duniani ni azimio la umoja wa
mataifa namba 45/2006 la mwaka 1990 na kuwataka mataifa kuwaenzi wazee wote
duniani na kuwajali pamoja na kuboresha maisha yao.
Katika kongamano
hilo Katibu huyo Mkuu amewataka wazee washiriki wa kongamano hilo kujikita pia
katika kutoa maoni juu ya nini kifanyike katika kuwahudumia wazee na kuboresha
maisha yao baada ya kulitumikia taifa katika nafasi mbalimbali kwa kutoa
mapendekezo yatakayosaidia kuboresha
sera ya wazee.
Aidha amedai
kwa sasa serikali inafanya mapitio ya sera ya wazee na ametaka kongamano hilo
kuwa sehemu ya maoni ambayo yatasaidia kuboresha kwa kuwa washiriki wengi
wamatoka katika maeneo mbalimbali ya nchi hivyo kwa sasa ipo katika hatua ya
kukusanya maoni toka kwa wananchi na wazee wenyewe.
Katika
kongamano hilo miongoni mwa maoni ambayo wazee wameyatoa ni pamoja na kuiomba
serikali kuwawekea dawa zinazoendana na magonja ya wazee kwa kuwa kwa sasa katika
hospitali nyingi nchini zina ukosefu wa dawa kwa wazee hali ambayo inachangia
vifo visivyotarajiwa.
“Tunaiomba
serikali iangalie suala la madawa yanayoendana na magonjwa ya wazee kwakuwa
mara nyingi tunakosa dawa mahospitalini na kusababisha vifo vya wazee hapa
nchini kuongezeka,”amesema Hafsa Kiyasile.
Pia kuhusu
suala la wazee kuondolewa katika makundi maalum ambayo yananufaika na mambo
mbalimbali kama vile mikopo,jambo hilo linaleta simanzi kwao na wameitaka
serikali kuwaweka kama yalivyo makundi ya wanawake,vijana na walemavu ili nao
wastahili mikopo kama haya makundi yanavyonufaika.
Wamependekeza
wazee wapewe pensheni kila mwezi kama ilivyo Zanzibar .
Comments
Post a Comment