Papa: Tunafanyia uchunguzi kashfa ndani ya Kanisa

BAba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Mexico hivi karibuni pamoja na mambo mengine amezungumzia mauaji ya wanawake ndani ya familia, ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji; uhusiano kati ya siasa na uchumi; madhara ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.
Hii ni sehemu ya tafakari ya kina kuhusu hali halisi ya kimataifa sanjari na maisha na utume wa Kanisa kadiri anavyoufahamu Baba Mtakatifu Fransisko.
Kuhusu shutuma za kashfa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza ndani ya Kanisa, Baba Mtakatifu amesema kuwa, wanazifanyia kazi na kwamba, si kila kitu lazima kitolewe hadharani. Lazima uchunguzi ufanyike na kujiridhisha.
Pia Kanisa lina nidhamu ya kuendesha kashfa na kwamba halifanyii kazi story za mitandao na maneno ya kuambiwa. Lazima lifanye uchunguzi wa kina.
Jambo la msingi ni watu kuwa na uvumilivu, ili kutoa nafasi kwa viongozi wa Kanisa kufanya uchunguzi wa kina na matokeo kutolewa kwa wakati.
Aidha amefafanua kuwa pale viongozi wa Kanisa wanapopatikana na hatia, hatua za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa mara moja.
 Wakati mwingine, Kanisa linalazimika kukaa kimya kama alivyofanya Yesu na hapo ni mwanzo wa watu kuchunguza dhamiri zao ili hatimaye, kuibuka na majibu muafaka.
 Mkutano wa Kanisa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo umekuwa na mafanikio makubwa na wengi wameridhishwa na jinsi mambo yalivyoendeshwa.
Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia;  anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.
Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Kanisa litaendelea kuwa ni Mama na Mwalimu kwa kukazia toba na wongofu wa ndani, ili watoto wake waweze kuchuchumilia utakatifu wa maisha.
Pia Papa Fransisko amesema kuwa, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya maskini na Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.
Kanisa litaendelea kuhamasisha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia kwa kutambua kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi lisiliokuwa na alama. Mambo makuu manne yanayozingatiwa na Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha. Wakimbizi na wahamiaji wakiheshimiwa na kuthaminiwa wanaweza pia kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi wahisani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa litaendelea kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini au “Eutanasia”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema si kwamba, Kanisa linahalalisha matendo yao ambayo ni kinyume cha mpango wa Mungu. Mafundisho msingi ya Mama Kanisa kuhusu ndoa na familia ni kama yanavyofafanuliwa kwenye Katekesimu ya Kanisa Katoliki ma Wosia wa Kitume: Furaha ya Upendo ndani ya familia ”Amoris Laetitia” ni habari njema kwa familia ya Mungu. Katika maisha na utume wake, ataendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Mafundisho ya Kanisa bila kupepesapepesa macho! Hakuna ndoa ya watu wa jinsia moja!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU