Ask. Nyaisonga: Kanisa litumie vyombo vya habari kuinjilisha

Na Thompson Mpanji, Mbeya
WAUMINI  wa Kanisa Katoliki  wamealikwa   kuhubiri habari njema kupitia teknolojia mpya ya mawasiliano .
Teknolojia ya sasa mathalani redio, runinga, mitandao ya kijamii ambapo watu wa kizazi hiki wamehamia humo ndiyo nyenzo pekee muhimu  inayoweza kutumika  kufikisha ujumbe wa Injili.
Hayo yameelezwa na  Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,Mhashamu Gervas Nyaisonga katika homilia yake  wakati wa adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa harambee ya  mbio za Mama Maria(Mariathon ) ambapo Radio Maria Tanzania ilifanya uzinduzi huo  kijimbo Mei 5 mwaka huu  katika Kanisa la Mtakatifu Patrick,Parokia ya Vwawa,Mbozi.
 Kwa Mujibu wa Mwakilishi wa Radio Maria Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,Thobias Mihale lengo ya harambee  hiyo ni kukusanya Sh.Mil.35 kwa mwezi mei,ambapo katika  uzinduzi huo  zaidi ya Sh.Mil.2.3 taslimu zilipatikana baada ya kuchangwa na waumini pamoja na   marafiki wa Radio Maria jimboni humo.
Askofu Nyaisonga   amewaalika waamini  kutumia nafasi ya kutafakari  sababu  ya kupewa kila mmoja kipawa  kwa makusudi yake  na kuwasihi waweze kuvitumia kadri ya mapenzi yake mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutangaza na kueneza habari njema.
“Kila mmoja wetu ameumbwa  na kupewa karama yake  ili tuweze kutangaza habari  njema ya Mungu na watakaoamini waweze kubatizwa  ili waweze kupata uzima wa milele na kwamba  hilo ndiyo  kusudio la juu ama wito mkuu  wa  kuwafanya watu wote waweze kupata wongofu kupitia habari   njema,”amefafanua Askofu Mkuu Nyaisonga.
 Amesema kuwa tendo la uenezaji wa habari njema  linakwenda kwa nyakati ambazo katika zama zilizopita  wamisionari waliweza kutumia karama zao  kupita kuhubiri habari njema kwa wayahudi na mataifa kwa  kutumia usafiri wa mnyama aina ya  Punda uliowawezesha kusafiri  umbali mrefu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Nyakati zetu ni tofauti. Tutake tusitake teknolojia ya habari na mawasiliano  ndiyo nyenzo ya sasa hatuwezi  kurudi kwenye zile zama za kusafiri kwa kutumia punda walivyofanya wamisionari  miaka 150 iliyopita kuwafikia watu  na waliwafikia wachache lakini sasa wanatakiwa  wafikiwe wengi  kwa wakati,” amefafanua zaidi Askofu Mkuu Nyaisonga.
 Ni nyenzo ambayo inawafikia  walio wengi  kwa muda mfupi na muda muafaka  kile ambacho unachokiamini, unachokipenda kiweze kufikiwa na kupokelewa na wengi  kipate mashabiki wengi kama vilivyo vilabu vikubwa nchini Tanzania Simba na Yanga ambavyo vimekuwa vikipata na kupendwa na  mashabiki wengi ni lazima kuwe na nyenzo  na nyenzo ni hizo haitoshi tu tukigawa  na kuuza vitabu  na misalaba,kwanza  sisi hatuna desturi ya kusoma vitabu,” Amesema  Mhashamu Askofu Mkuu Nyaisonga.
 “Lazima habari njema itangazwe,yatolewe mafundisho,waamini waijue Katekisimu…habari njema itangaze ili watu iwachome kwenye dhamiri zao kama wale wazee wa makuhani…itangazwe wasikie hata wasipokusikia leo watasikia kesho na kesho kutwa  ndiyo maana wanakwaya wanaendelea kuimba kesho na keshokutwa na namna nzuri wasikie kwenye radio,wasikie kwenye nyenzo nyingine  wasome kwenye  magazeti ,wasikie kwenye vyombo vingine.
Leo tupo hapa wapo wagonjwa  mahospitalini na majumbani,wazee na wasio jiweza kufika  hapa ,walioshindwa kuja hapa  kwa sababu mbalimbali wasikilize kwenye Radio neno la mungu,mimi siwezi kwenda sokoni kuhubiri lakini  wapo nitakaowatuma kwenda kutangaza kupitia  karama zao kwa kutumia nyenzo kama vyombo vya habari.

 Kwa hiyo wakatoliki ndugu zangu tuna wajibu  wa kushuhudia tunachoamini…kutokutangaza  maana yake hata imani yenyewe ina dosari. Tuna wajibu wa kusimama kidete  na kusema kwamba ,ninaamini  kwamba huyu aliyechinjwa,huyu ambaye ni  pasaka yake ninaishangilia ,huyu aliyechinjwa anastahili uweza na nguvu hakuna muweza  mwingine, hakuna mwenye nguvu mwingine  ,ni huyu huyu anastahili uweza na nguvu  na ndiye atakayenipa nguvu mimi ,”amesisitiza Askofu Mkuu Nyaisonga.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU