Ask Msonganzila aonya juu ya migogoro katika familia


Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Michael Msonganzila akibariki  msingi  wa Kanisa linalojengwa lenye uwezo wa kuchukua waamini zaidi ya 1500 kwa wakati mmoja,katika kigango cha Bisumwa Parokia ya Kigera Jimboni humo wakati wa ziara yake ya kichungaji katika Parokia hiyo Mei 02 hadi 05 mwaka huu.(Picha na Veronica Modest)
Na Veronica Modest, Kigera Musoma.
askofu wa Jimbo Katoliki  Musoma Michael Msonganzila amesema  migogoro ya mara kwa mara,wizi  na kiburi ni kutokana na waamini kujisahau kuwa wameumbwa kwa mfano wa Sura ya Mungu na hivyo kufanya vitu visivyoendana na tabia za Mungu.
Askofu Msonganzila ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kichungaji katika Parokia ya Kigera ambapo alitembelea kigango cha Buruma na kubariki Kanisa jipya na kufungua  jiwe la msingi.
Akiwa katika kigango cha Bisumwa alibariki msingi wa Kanisa kubwa lenye uwezo wa kuchukua waamini zaidi ya  1500 kwa wakati mmoja na kutoa Sakaramenti ya Kipaimara kwa waamini zaidi ya 390 katika Parokia hiyo.
“Wizi unatoka wapi, kutokuwajibika mahali pa kazi kunatoka wapi nataka moyo unaokujika moyo wa unyenyekevu, unaobondeka na kukunjwa kwa neno la Mungu dunia yetu tunaifahamu ilivyo kwa sasa watu tumejaa kiburi,hakuna nidhamu kwa wazazi,hakuna utii kati yenu ninyi wenyewe
Hii sura ya Mungu tunaipeleka wapi kwa nini mapigano kila mara, katika familia hakuna utulivu na watoto wanajifunza nini kutoka kwenu wazazi,hata majirani hatukai nao kwa amani, tuheshimu sura hiyo,”amesema Askofu Msonganzila.
 Amewataka vijana waliopata sakramenti ya Kipaimara kuhakikisha wanakuwa waalimu na wahusika wa kusikiliza na kushikiria  neno la Mungu kikamilifu kwa matendo na majitoleo katika kufanya kazi ya Mungu, na kutokuruhusu kupotoshwa imani yao ya Kanisa Katoliki,kwani vijana wengi wamekuwa wakipotoka kwa kuhamia makanisa mengine na kuacha imani yao waliyobatizwa na kupokea sakramenti zote za awali.
 Amewapongeza waamini wa Parokia hiyo kwa kuhakikisha kazi ya Mungu inasonga mbele mbali ya changamoto mbalimbali za maisha wanazokumbana nazo,ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maeneo yote ya Kanisa wanatunza kumbukumbu vizuri kwa ajili ya faida yao na  kizazi kijacho ,ili kuondoa migogoro ya ardhi ambayo inaweza kuibuka hapo baade.
 Paroko wa Paroki hiyo Padri Robert Luvakubandi amesema ziara ya Askofu wa Jimbo la Musoma katika Parokia yake itasaidia sana kuimarisha waamini kiroho na hata kuwaongezea nguvu ya imani wale ambao walikuwa wanataka kulegea na kurudi yuma kiimani.
Paroko huyo aliwapongeza waamini wa kigango cha Buruma,Bisumwa na Parokia ya Kigera kwa ushirikiano wao mzuri wanaounyesha katika kukua kiimani, hasa katika ushiriki wao  wa ujenzi wa makanisa unaoendelea katika maeneo yao kwa kuwa wamejitoa kwa hali na mali katika kutoa michango yao ya kifedha na nguvu kazi.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU