Askofu Kassala kutoa rehema kamili kwa wanahija Geita

Na Salvatory Magangira
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amesema atatoa Rehema Kamili  “Indulgensia” kwa wanahija watakaohiji katika Kituo cha Hija cha Nyamatongo Parokiani Nyantakubwa jimboni humo.
Akizungumza katika Misa Takatifu ya Ushemasi wa Frateli Albert Warioba wa Jimbo Katoliki Geita, Askofu Kassala amesema anatumia uwezo wake aliopewa na Baba Mtakatifu kutoa rehema kamili kwa baadhi ya wanahija watakaokidhi  vigezo Juni 15 mwaka huu vikiwemo kufanya majuto kamili, kuungama dhambi na kupokea Ekaristi Takatifu na kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu.
Kituo hicho kilizunduliwa rasmi mwaka 2017 katika kuadhimisha miaka 100 ya Upadri Tanzania ambapo Waamini wa Jimbo la Geita walichagua kituo cha Nyamatongo kwa kuwa juu ya Kilima hicho alifariki Padri Pierre Combarieu na kuzikwa hapo mwaka 1881 baada ya jaribio la kuanzisha Misheni (Parokia) mahali hapo kukwama.
Miongoni mwa vivutio vinavyochochea mwamko wa kiimani katika Kilima hicho ni Msalaba mkubwa ulioachwa hapo na wamisionari tangu mwaka 1881 na kaburi la padri huyo lisiloonekana mahali hapo.
Wenyeji wa eneo hilo akiwemo mjukuu halisi wa Mtemi Rwoma aliyewapa wamisionari wa Kifaransa wa shirika la White Fathers ardhi hiyo ambaye bado yupo hapo jina lake Gabriel Rwoma amesisitiza kuwa eneo liliheshimiwa lisivamiwe na mtu yeyote mbali ya kuachanizwa kwa zaidi ya miaka 138.
kwa tamko lake la kuanza kutoka rehema kamili ambayo ni msamaha kamili wa adhabu za dhambi zote mtu alizotenda kila mwaka kwa washiriki wa hija watakaokidhi vigezo, Askofu Kassala ameipandisha hadhi hija ya mwaka huu ambapo mamia ya mahujaji wanategemewa kushiriki, wakiwemo wanakwaya ambao hufanya mashindano ya nyimbo na kuchangamsha tukio zima.
Hija hiyo ya Kijimbo iliyoidhinishwa na Askofu Kassala muda mfupi tu baada ya kusimikwa Jimboni Geita imezidi kuchukua umaarufu baada ya waamini kutoka parokia zote za Jimbo hilo na baadhi kutoka Jimbo Kuu Katoliki Mwanza kukubali kumiminika kwa wingi kushudia maajabu ya kilima hicho kila mwaka kwa kusali Misa takatifu, kupata semina za kiroho, kitubio na mafungo.
Wakizungumza kwa nafasi tofauti waamini wa Jimbo Katoliki Geita wameahidi kushiriki hija hiyo kwa wingi ijapokuwa baadhi wamekiri hawakuwahi kufahamu nini maana ya rehema kamili na hivyo kuwaomba mapadri watoe elimu ya kutosha wakati wa mahubiri Kanisani ili waamini walewe zaidi jambo hilo.



Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU